Papa kutembelea kituo cha kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji mjini Roma
Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Kituo cha Kuhudumia Wakimbizi kinachoendeswa
na Shirika la Wayesuit hapa Roma, kama kielelezo cha mshikamano na wahamiaji na wageni
wanaokabiliwa na changamoto mbali mbali katika maisha wanapokuwa ugenini.
Taarifa
hii imetolewa na Shirika la Habari la ANSA baada ya kuthibitisha habari hizi kutoka
kwa Padre Giovanni La Manna, Mkurugenzi wa Kituo cha Kuhudumia Wakimbizi cha Wayesuit
kilichoko mjini Roma. Padre la Manna anasema, mara ya kwanza aliposikia simu ikidai
kwamba inatoka kwa Papa Francisko hakuamini na kwa kitambo kidogo alipigwa na bumbuwazi.
Itakumbukwa kwamba, wakati wa baraka na ujumbe wake kwa mji wa Roma na Dunia
kwa ujumla, Baba Mtakatifu aligusia kwa namna ya pekee umuhimu wa kusimama kidete
kulinda na kutetea haki, amani, upendo na mshikamano. Kunako mwaka 1980 Padre Pedro
Arrupe, Mkuu wa Shirika la Wayesuit kwa wakati huo, alianzisha Shirika la Kuhudumia
Wakimbzi, ambalo hadi sasa linatekeleza utume wake katika nchi 40. Limekuwa mstari
wa mbele kutetea haki msingi za wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum.
Jijini Roma, kituo hiki kinatoa chakula kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji.
Kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Kituo cha Kuwahudumia Wakimbizi cha
Wayesuit ni kielelezo cha mshikamano wa Kanisa kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii.