Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Ulimwenguni, jumanne tarehe 8 Aprili 2013
limefungua mkutano mkuu wa Vyama vya Wanawake Wakatoliki kutoka Amerika ya Kusini
na nchi za Caribbean, unaofanyika Jijini Mexico na unatarajiwa kufungwa rasmi hapo
tarehe 12 Aprili 2013. Wajumbe wanapembua kuhusu biashara haramu ya binadamu duniani.
Mama
Maria Giovanni Ruggieri, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Ulimwenguni
anasema, wanapania pamoja na mambo mengine kuwafahamisha Wanawake na wadau mbali mbali
kuhusu athari za biashara haramu ya binadamu inayoendelea duniani. Hili ni jukumu
kwa kila mtu kusimama kidete kuhakikisha kwamba, biashara hii inatokomezwa katika
uso wa dunia.
Chama hiki kinapenda kutoa mchango wake katika harakati za kutokomeza
biashara haramu ya binadamu inayoendelea kukua na kushamiri siku hadi siku. Huu ni
uvunjaji wa haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anaonekana kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, mwenye haki zake msingi
zinazopaswa kuheshimiwa na kulindwa kwa udi na uvumba.
Wajumbe wanaendelea
kuchambua maana ya biashara haramu ya binadamu, chanzo chake, wahusika wakuu na mitandao
yao pamoja na dhamana ya serikali husika katika kudhibiti na hatimaye kukomesha biashara
haramu ya binadamu. Kuna uhusiano mkubwa kati ya uhamiaji na biashara haramu ya binadamu
pamoja na aina mbali mbali za dhuluma na nyanyaso za kijinsia zinazoendelea kujionesha
sehemu mbali mbali ya dunia.
Wajumbe watafahamishana sera na mikakati iliyoibuliwa
na Vyama mbali mbali vya kitume kama sehemu ya mchakato wa kupambana na biashara haramu
ya binadamu; pamoja na kuwasaidia waathirika wa janga hili kuanza upya maisha yenye
matumaini mapya.
Wajumbe watapata fursa pia kupembua hatua za ushirikiano
zilizopo katika ngazi mbali mbali. Mwishoni, wajumbe watapata nafasi ya kuangalia
mchango wa vyombo vya upashanaji wa habari katika mapambano dhidi ya biashara haramu
ya binadamu.