2013-04-08 11:38:11

Watanzania jengeni utamaduni wa majadiliano ili kudumisha misingi ya haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa!


Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania anabainisha kwamba, Kanisa linatambua na kuthamini misingi ya haki, amani na upatanisho katika maisha na maendeleo ya watu. RealAudioMP3

Kwa bahati mbaya katika Jamii kuna watu ambao kwa makusudi mazima au kwa kutoelewa kwao wameshindwa kuthamini amani na utulivu nchini Tanzania. Matokeo yake ni: malumbano, kinzani na choko choko za kidini zinazofanywa na waamini wenye misimamo mikali ya kiimani.

Mazingira kama haya yanaweza kuwajengea baadhi ya watu hisia za chuki, uhasama na hali ya kutaka kulipiza kisasi. Kanisa bado linaendelea kuwahamasisha waamini na watanzania wenye mapenzi mema kujikita katika kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa kwa ajili ya mafao ya wengi. Kamwe wasiingie kwenye kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi, kwani vita haina macho, watakaoathirika zaidi ni wale watu ambao hawana hatia.

Kuna haja kwa watanzania anasema Askofu mkuu Josephat Lebulu kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene, wote wapanie kutafuta amani na upatanisho kwani ni heri wapatanishi maana wao wataitwa ni wana wa Mungu. Watanzania watafute mambo yanayopelekea chokochoko na kinzani za kidini; tofauti zao za kimsingi na kubainisha hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa ili kuendeleza misingi ya haki, amani na utulivu nchini Tanzania. Wananchi washinde ubaya kwa kutenda wema.

Askofu mkuu Josephat Lebulu akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni kuhusu Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Ukristo Jimbo kuu Katoliki Arusha, alisema, Kanisa katika mikakati yake linapenda kutumia fursa hii kusali kwa ajili ya kuombea amani, utulivu na upatanisho wa kweli. Maadhimisho ya Jubilee ya Ukristo yanakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na hatimaye, kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, changamoto ya kumwilisha imani katika matendo.

Waamini kwa wakati huu watatembeza Msalaba wa Jubilee katika Familia, Jumuiya na Parokia zote za Jimbo kuu la Arusha. Kilele cha Maadhimisho ya Jubilee hii ni hapo Desemba 2013. Ni matumaini ya Askofu mkuu Lebulu kwamba, Kanisa kuu la Jimbo kuu la Arusha litakuwa limekamilika na waamini wataweza kusali humo ili kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani. Jimbo kuu la Arusha lina matatizo, fursa na changamoto ambazo linaendelea kuzifanyia kazi katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, ili kuhakikisha kwamba, Uinjilishaji wa kina unagusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.







All the contents on this site are copyrighted ©.