Simameni kidete kutetea zawadi ya uhai, maadili, utu wema na utunzaji bora wa mazingira
Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini, limewaandikia waamini Barua ya kichungaji
likiwataka kusimama kidete katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya magumu
na vikwazo vingi wanavyoendelea kukabiliana navyo katika hija ya maisha yao kama waamini.
Mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini ulitanguliwa na semina
maalum kuhusu tasaufi ya utumishi pamoja na urithishaji wa imani, kama walivyofafanua
Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya.
Maaskofu pia wameangalia
utekelezaji wa mikakati ya Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 500 tangu Ukristo ulipoingia
nchini humo, kipindi cha miaka tisa kuanzia sasa. Mkutano huu ulifunguliwa kwa salam
na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, yaliyotumwa kwa
niaba yake na Kardinali Tarcisio Bertone, katibu mkuu wa Vatican na kusomwa na Askofu
mkuu Giuseppe Pinto, Balozi wa Vatican nchini Ufilippini.
Maaskofu wameonesha
mshikamano wao wa dhati na wananchi wa Ufilippini walioathirika kutokana na tufani
zilizowakumba kwa siku za hivi karibuni, kiasi cha kusababisha maafa makubwa nchini
humo. Watu wengi wamepoteza maisha, mali pamoja na miundo mbinu kuharibiwa vibaya.
Maaskofu wanasema kwamba, athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazoendelea kuleta
maafa makubwa nchini humo na sehemu nyingine duniani ni matokeo ya binadamu kutozingatia
sheria na kanuni za utunzaji bora wa mazingira.
Kuna ukataji ovyo wa miti
pamoja na uchimbaji mbaya wa madini, usiozingatia mafao ya wengi na badala yake, wawekezaji
wanajikuta wakielemewa zaidi na faida, kuliko hasara zinazoweza kujitokeza kwa siku
za baadaye. Maafa yote haya ni changamoto kwa wananchi na viongozi nchini humo kufanya
tafakari ya kina kuhusu ukweli, ubora na tija inayotolewa na viongozi hawa kwa ajili
ya mafao ya wengi, kama sehemu ya mchakato wa uwajibikaji na utendaji makini wa shughuli
za uongozi.
Licha ya maafa makubwa yaliyosababishwa na tufani hizi, lakini
pia wananchi wa Ufilippini wanakabiliwa na maafa makubwa kutokana na baadhi ya viongozi
wao wanaokumbatia utamaduni wa kifo kwa kutaka kuiga sera na vipaumbele vya Nchi za
Magharibi, ambavyo wakati mwingine vinasigana na maadili na utu wema. Baadhi yao wamejikuta
wakizama katika rushwa, ufisadi na ubadhilifu wa mali ya umma, kwa kujiundia makundi
ya wanasiasa wanaojitafuta badala ya kutafuta mafao ya wengi.
Ni changamoto
ya kuwa waaminifu katika kanuni za uongozi, daima wakitafuta Haki Jamii, Mafao ya
Wengi pamoja na kukumbatia zawadi ya maisha. Ni jambo lisilokubalika kwamba, kuna
watu wanaendelea kupoteza maisha yao, kutekwa na kubakwa, wakati kuna sheria na vyombo
ambavyo vinapaswa kusimamia sheria na kanuni za nchi. Kuna haja kwa viongozi wa namna
hii kuwajibishwa barabara, ili haki, amani na utulivu viweze kutawala tena miongoni
mwa wananchi wa Ufilippini.
Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linasema,
msimamo wa Kanisa Katoliki ni kuendelea kutetea zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa
mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa
Mungu. Hawakubaliani na sera na sheria za afya ya uzazi zinazotaka kukumbatia utamaduni
wa kifo pamoja na kupelekea kumong’onyoka kwa maadili na utu wema nchini humio kwa
kizingizio cha kutaka kupata misaada ya kiuchumi.
Maaskofu wanasema, rushwa,
ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma ni kati ya majanga makubwa yanayodhalilisha
utawala bora na uongozi wa sheria. Ikumbukwe kwamba, viongozi wanapaswa kusimamia
mafao ya wengi na nafasi za uongozi walizokabidhiwa na jamii si kwa ajili ya kujitafuta
na kwa ajili ya masilahi yao binafsi. Wananchi wawe makini katika kuwaangalia viongozi
wa aina hii na wawe na ujasiri wa kuwanyima kura wakati wa uchaguzi mkuu.
Maadili
na utu wema, upendeleo kwa maskini ni kati ya mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa
pekee ili kuleta maboresho ya maisha ya wananchi wengi wa Ufilippini wanaoogelea katika
umaskini wa kipato, kinzani na migogoro ya kijamii. Waamini na wananchi kwa ujumla
wajitahidi kufuata dhamiri zao nyofu na kamwe wasikubali kushinikizwa kutenda mambo
ambayo yako kinyume cha dhamiri nyofu, utu na maadili mema.
Maaskofu hali wameshikamana
na Khalifa wa Mtakatifu Petro wanasema, wataendelea kutangaza ukweli na kutweka hadi
kilindini, pasi na woga wala wasi wasi katika maji marefu yanayoonesha kukengeuka
kwa binadamu. Kanisa linafanya yote haya likisukumwa na imani, maadili na utu wema,
daima likitafuta mafao ya wengi.
Kanisa linaendelea kuhimiza waamini na wananchi
katika ujumla wao kufuata njia ya mpango wa uzazi asilia, unaoheshimu zawadi ya maisha
na kuwawajibisha wanandoa, kama sehemu ya kuenzi Injili ya Maisha. Vijana wajitahidi
kujizuia, kusubiri na kuwa waaminifu katika mahusiano yao, wakitambua kwamba, bado
Ukimwi ni janga la Kimataifa.
Maaskofu wanaipongeza Serikali kwa hatua mbali
mbali zilizochukuliwa nchini humo katika kulinda na kudumisha haki, amani na utulivu
na kwamba, amani ni matunda ya haki. Kanisa, litaendelea kuwa ni sauti ya kinabii
kwa: maskini, wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Mwishoni wanasema,
wote hawa hawana budi kutangaziwa kweli za Injili zinazogusa undani mwa mtu: kiroho
na kimwili.