2013-04-08 15:41:03

Rais wa Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri nchini Ujerumani akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu amekutana na kuzungumza na na Mheshimiwa Nikolaus Schneider, Rais wa Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri nchini Ujerumani.

Akizungumzia tukio hili, Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Mheshimiwa Schneider, amempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa na kwa namna ya pekee, jina ambalo ni kama dira na mwongozo wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatofu Petro kwani jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi ni jina lenye mvuto na mashiko kwa Wakristo wengi sehemu mbali mbali za dunia.

Viongozi hawa wawili wamezungumzia pia shida na mahangaiko ya wananchi wa Argentina waliokumbwa na mafuriko hivi karibuni na kusababisha maafa makubwa, jambo ambalo limewagusa viongozi hawa wawili na kuonesha moyo wa mshikamano na upendo kwa wote walioathirika.

Majadiliano ya kiekumene yamelenga zaidi ushuhuda wa imani unaooneshwa na wafiadini wa Kikristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Viongozi hawa wanatambua mateso na mahangaiko ya waamini wao walioteswa na kudhulumiwa nyakati za tawala za kidhalimu.

Wanasema, damu ya mashahidi hawa wa imani ni jambo linalowaunganisha Wakristo kutoka Makanisa mbali mbali ili kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa la Kiinjili la Kiluteri linajiandaa kuadhimisha tukio la kihistoria la mageuzi ndani ya Kanisa litakalofanyika kunako mwaka 2017.

Papa Francisko amekumbushia hotuba ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliyoitoa mjini Erfurt, mahali alipozaliwa na Martin Luther na kutekeleza utume wake ndani ya Kanisa, changamoto ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene baina ya Makanisa haya mawili mintarafu mapokeo ya Mageuzi yaliyoletwa na Martin Luther. Mazungumzo baina ya viongozi hawa wawili anasema Padre Lombardi yamekuwa na manufaa makubwa baina ya Makanisa haya mawili.







All the contents on this site are copyrighted ©.