2013-04-08 10:45:26

Papa Francisko asimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo la Roma


Baba Mtakatifu Francisko,jioni ya Jumapili ya huruma ya Mungu, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kusimikwa rasmi kuwa ni Askofu wa Jimbo kuu la Roma. Mwanzoni mwa Ibada, wawakilishi wa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma walionesha utii kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Hawa ni Kardinali, Askofu msaidizi, Paroko na Paroko Msaidizi; Shemasi, Mtawa, Familia na Vijana wawili. Ibada hii ya Misa takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano ambayo kimsingi ni Makao Makuu ya Jimbo kuu la Roma.

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko ameishukuru Familia ya Mungu Jimboni Roma na kuitaka kuonja upendo wa Mungu unaojionesha kwa namna ya pekee katika huruma ya Mungu inayowaelekeza, kuwainua pamoja na kuwaongoza. Hii ndiyo ile huruma na uvumilivu iliyooneshwa na Yesu kwa Mtume Tomaso ambaye alikuwa na imani haba, anamsubiri kwa juma zima na wanapokutana Mtume Tomaso anatambua umaskini wake wa kiroho na uhaba wa imani, aliyokuwa nayo, licha ya ushuhuda uliokuwa umetolewa na Mitume wengine.

Bwana wangu na Mungu wangu, ni ungamo la imani linalojibu uvumilivu wa Yesu kwa wafuasi wake, Tomaso anabahatika kuwa ni mtu mpya na mwenye imani thabiti. Itakumbukwa kwamba, hata Mtume Petro alimkana Yesu mara tatu, lakini alipokutana na Yesu, akamwimaarisha katika imani licha ya mapungufu yake ya kibinadamu, jambo la msingi alilopaswa kutenda ni kumwamini Yesu. Petro mtume, alionja upendo wa Yesu alipomwangalia, kiasi cha kutokwa na machozi, yote haya yanaonesha huruma ya Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu anaendelea kuonesha jinsi ambavyo huruma ya Mungu imeweza kuwasindikiza wafuasi wake kiasi hata cha kuweza kukomaa katika imani, kama ilivyojitokeza pia kwa wale Wafuasi wa Emmaus. Hii ndiyo hulka ya Mungu inayofanya mambo kwa wakati na sio kama binadamu anayetamani kupata yote kwa mkupuo!

Mungu anapenda, anaelewa na kutumaini, kamwe hawezi kuwaacha waja wake, anafahamu kusamehe; anaendelea kusubiri kwa subira, hata pale waamini wanapotokomea na kutopea kwenye dhambi; pale wanapotubu na kumrudia tena, yuko tayari kuwaonjesha huruma yake na kuwakumbatia kwa upendo.

Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo ile huruma ya Mungu inayojionesha katika Simulizi la Baba mwenye huruma anayeonesha matumaini ya ajabu hata kwa mtoto wake mdogo aliyetapanya mali yake ya urithi, alipotubu na kumrudia Baba yake, alionja kwa mara nyingine tena: upendo, huruma na furaha ya kweli hata baada ya kutapanya uhuru wake kwa mambo ya ovyoo! Mwenyezi Mungu anajibu udhaifu wa mwanadamu kwa njia ya uvumilivu, chemchemi ya imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anaonya kwamba, ili huruma ya Mungu iweze kupata makazi katika maisha ya mwamini kuna haja ya mwamini mwenyewe kuwa na ujasiri, nia na utashi wa kumrudia Mungu ili kuweza kujificha katika Madonda Matakatifu ya Yesu, chemchemi ya upendo usiokuwa na kifani, hata kama wanaelemewa na mzigo wa dhambi kiasi gani! Mwenyezi Mungu anamsubiri kila mtu mmoja mmoja anapoonesha nia na ujasiri wa kumrudia Mungu anayemwangalia kila mtu katika nafsi yake na wala si kama makundi ya watu!

Mwamini anapoelemewa na dhambi, awe na ujasiri wa kumrudia Mungu, ili aweze kusafishwa dhambi zake na hatimaye, kuonja: msamaha, huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Fadhila hizi zimeoneshwa na watu wengi anasema Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake alipokuwa anatekeleza shughuli mbali mbali za kichungaji.

Jambo la msingi ni kuwa na ujasiri wa kukimbilia kwenye Madonda Matakatifu ya Yesu, ili kujificha humo; ili kusafishwa dhambi kwa Damu Azizi ya Yesu Kristo. Daima Mwenyezi Mungu, atampokea na kumkaribisha mja wake; atamwosha, mfariji na kumpenda.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake katika Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kwa kuwaalika waamini kuendelea kutumainia huruma ya Mungu, kuwa na utashi na ujasiri wa kurudi nyumbani kwa Baba yao wa mbinguni ili kuonja msamaha, huruma na upendo wake unaobubujika kutoka katika Madonda Matakatifu ya Yesu.

Ni mwaliko wa kuikimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, kwa njia hii, waamini pia watawezeshwa kuwa kweli ni vyombo vya huruma, uvumilivu, msamaha na upendo wa Mungu.

Mara baada ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko alipanda kwenye Sebule ya Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kwa ajili ya kuwasalimia waamini na watu wenye mapenzi mema waliokuwa wamejitokeza kwa wingi mbele ya Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano.

Kwa mara nyingine tena amewaomba kuendelea kumsindikiza katika sala na maombi yao, wakiandamana kwa pamoja, yaani Askofu na Waamini wake wakishuhudia furaha ya Kristo Mfufuka anayetembea pamoja nao katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Kabla ya Ibada ya Misa Takatifu Baba Mtakatifu Francisko alizundua Nembo ya Mtaa kwa ajili ya kumbu kumbu ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili. Heshima hii imetolewa na Manispaa ya Jiji la Roma kwa kutambua mchango mkubwa uliotolewa na Papa Yohane Paulo wa pili enzi ya uhai wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma.







All the contents on this site are copyrighted ©.