Familia za Kikristo katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani
Tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, kumekuwepo
upepo tofauti unaovuma kukazia umoja, upendo na mshikamano wa dhati; imani na matumaini
kwa wale waliokata tamaa pamoja na ushuhuda wenye mvuto kwa Kristo na Kanisa lake.
Ni maneno ya
Askofu Mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia katika hafla fupi
ya maboresho ya tovuti ya Baraza lake na Jarida ambalo linatolewa katika lugha nne
za kimataifa kwa ajili ya Familia, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku
ya Nane ya Familia Kimataifa, itakayofanyika Jijini Philadelphia, kuanzia tarehe 22
hadi tarehe 27 Septemba 2015. Hili ni tukio la Kikanisa linalozihusisha familia
za kikristo katika maisha na utume wake. Familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia
zimeanza pia maandalizi kwa ajili ya kushiriki katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani
kwa kuungana na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 26 hadi 27 Oktoba 2013 ili kumwimbia
Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi kubwa ya Familia. Itakuwa ni
fursa kwa familia hizi kuweza kuimaarisha imani yao kwa kutembelea Makaburi ya Miamba
wa Imani hapa Mjini Roma. Katika mkutano wa Baraza la Kipapa la Familia uliofanyika
hivi karibuni, baadhi ya wajumbe walionesha kuguswa na mtindo wa maisha na utume wa
Baba Mtakatifu Francisko hadi sasa, lakini pia wakaonesha wasi wasi wao kuhusu changamoto
mbali mbali anazopaswa kukabiliana na zo katika kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho
ya dunia. Wanasema, bado ulimwengu wa wanasiasa unaendelea kumsoma kwa umakini mkubwa;
hali ya kutovumiliana pamoja na utengenezaji wa sera ambazo kimsingi zimekuwa na ukakasi
mkubwa katika maisha na utume wa Familia katika Jamii. Katika kipindi cha miaka
kumi iliyopita, Kardinali Jorge Bergoglio amekuwa ni rejea makini ya miakati ya kichungaji,
maisha adili na utu wema nchini Argentina. Ni kiongozi ambaye anatoka katika kundi
la Mapadre vijana kutoka Amerika ya Kusini waliokuwa na ari, moyo na shauku ya kuleta
mabadiliko: kiroho na kimwili, kwenye miaka ya sitini na sabini; matunda ya Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican, moto wa kuotea mbali! Ni Kiongozi aliyesimama kidete
kulinda na kuwatetea wanyonge waliokuwa wanaelemewa na athari za myumbo wa uchumi
nchini Argentina; hali iliyopelekea idadi kubwa ya wananchi wa Argentina kuikimbia
nchi yao na kuhamia ugenini ambako walijikuta wakiwa ni wahamiaji. Baba Mtakatifu
Francisko ni kiongozi ambaye hadi sasa kwa maneno na matendo yake ni Baba mwenye huruma
anayesahihisha, anayetangaza na kukanya pale watoto wake wanapoonekana kutaka kuteleza
na kuanguka katika utupu wa mawazo na maisha! Uwepo wake ni kielelezo cha mwanga angavu
wa matumaini kwa watu waliokuwa wamekata tamaa. Huyu ndiye yule Msamaria mwema
anayeguswa na mahangaiko ya jirani zake, kiasi kwamba, anajishusha ili kuwaganga kwa
neno la faraja na uwepo wake unaoleta mguso! Kardinali Bergoglio anakumbukwa na
watu wengi nchini Argentina kama kiongozi aliyesimama kidete kulinda na kutetea: amani,
utulivu, haki msingi za binadamu na mafao ya wengi. Daima alipenda kusimamia utawala
wa sheria na kila mtu kuthaminiwa ili kuondokana na wasi wasi zisizo na msingi. Mtindo
huu wa maisha na utume kwa Kanisa, Kardinali Bergoglio ameacha deni kubwa kwa viongozi
mbali mbali nchini Argentina. Ni matumaini ya wajumbe wa mkutano wa Baraza la
Kipapa la Familia kwamba, ile dhamana ambayo Wakristo na watu wengi wenye mapenzi
mema wameonesha kwa kutaka kusali na kumwombea wataweza kutekeleza wajibu wao, ili
kweli Baba Mtakatifu Francisko aweze kutekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro kwa ufanisi mkubwa kadiri ya mapenzi ya Mungu mwenyewe.