Papa Tawadros II aonesha nia ya kukutana na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican
Patriaki Tawadros wa pili wa Kanisa la Kikoptik la Kiorthodox la Alexandria, Misri
ameonesha nia na utashi wa kutaka kukutana na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu
ya mchakato wa kuendeleza majadiliano ya kiekumene baina ya Makanisa haya mawili.
Hayo yamenukuliwa hivi karibuni na vyombo vya habari kutoka Misri.
Papa Tawadros
wa pili, hivi karibuni alikutana na kuzungumza na Askofu mkuu Jean Paul Gobel, aliyeteuliwa
hivi karibuni na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kuwa Balozi wa Vatican
nchini Misri. Katika mazungumzo ya viongozi hawa wawili, Papa Tawadros wa pili alionesha
nia ya kutaka kusafiri hadi mjini Vatican ili kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu
Francisko, ili kujenga na kuimarisha mshikamano wa kidugu baina ya Makanisa haya mawili.
Ikiwa
nia hii njema itaweza kutekelezwa, basi hili litakuwa ni tukio kuu la Kiekumene kuwahi
kutokea tangu mwaka 1973, wakati ambapo Papa Shenuda wa Tatu, alipokutana na kuzungumza
na Baba Mtakatifu Paulo wa sita mjini Vatican. Viongozi hawa wawili katika mazungumzo
yao walitoa tamko la pamoja kuhusiana na uelewa wa mafundisho juu ya Yesu na tangu
hapo wakaanzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene baina ya Makanisa haya mawili.