Mheshimiwa Padre Josè Rogriguez Carballo ateuliwa na Papa kuwa Katibu mkuu wa Baraza
la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Josè Rodriguez Carballo, Mkuu wa
Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa
la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu
mkuu.
Askofu mkuu mteule alizaliwa tarehe 11 Agosti 1953 nchini Hispania. Baada
ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kipadre, akapadrishwa kunako tarehe 28 Juni
1977 mjini Yerusalemu kwenye Kanisa la Mtakatifu Salvatori. Baada ya Upadrisho aliendelea
na masomo ya Sayansi ya Maandiko Matakatifu mjini Yerusalemu na Roma na kubahatika
kupata shahada ya Uzamivu katika Maandiko Matakatifu kunako mwaka 1981.
Tangu
wakati huo ametekeleza utume wake katika medani mbali mbali za maisha ya kitawa kama:
Mlezi wa Wanovisi, Mchumi, Katibu mkuu wa majiundo, Gombera, Jaalim. Kati ya mwaka
1992 hadi mwaka 1997 alikuwa ni Mkuu wa Kanda na Rais wa Wakuu wa Shirika la Wakapuchini
Barani Ulaya. Kunako mwaka 2003 akachaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wakapuchini na
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Antonianum, kilichoko mjini Roma. Mwaka 2012 alichaguliwa
kuwa Rais wa Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa Duniani.
Hadi uteuzi
wake, alikuwa ni mwanachama wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Baraza la
Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume na amekuwa mshiriki mzuri katika Maadhimisho
ya Sinodi za Maaskofu zilizofanyika kunako mwaka 2005, 2008, 2012 pamoja na Sinodi
Maalum ya Maaskofu Katoliki Mashariki ya Kati, iliyoadhimishwa mjini Vatican kunako
mwaka 2010.
Askofu mkuu mteule Josè Rodriguez Carballo ni mwandishi maarufu
wa vitabu na majarida kuhusu maisha ya kuwekwa wakfu, Taalimgu uchungaji, Maandiko
Matakatifu na Tasaufi ya Wafranciskani pia ni mtaalam aliyebobea katika lugha mbali
mbali za kimataifa.