2013-04-06 11:26:55

Kumbu kumbu ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda: 7 Aprili 2013


Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, katika mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda kunako mwaka 1994, watu zaidi ya millioni moja waliuwawa kikatili, na wanawake zaidi ya laki mbili na nusu walibakwa na kunyanyaswa kijinsia. Matukio yote haya yaliacha majonzi makubwa katika maisha ya wananchi wa Rwanda kwa kipindi kirefu.

Baada ya mauaji ya kimbari, Rwanda ilijipanga upya kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho, haki na amani. Jumuiya ya Kimataifa tarehe 7 Aprili 2013 inafanya kumbu kumbu ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda. Ni tukio ambalo limepita, lakini athari zake zimeacha kurasa chungu miongoni mwa wananchi wa Rwanda hata pengine na katika nchi majirani.

Kunako mwaka 1994 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliunda Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Rwanda, ili kusikiliza kesi za mauaji kwa watu waliokuwa wanatuhumiwa kujihusisha na mambo hayo ili haki iweze kutendeka. Mahakama hii ilihitimisha kazi zake kunako mwaka 2012. Watu 93 walishutumiwa kujihusisha na mauaji ya kimbari nchini Rwanda; kati yao 83 wamekwisha kukamatwa na kufikishwa mahakamani; 75 ya watuhumiwa wamesomewa mashitaka na kesi zao kuhukumiwa.

Watu 65 walipatikana na hatia na wengine 10 wakaachiliwa huru. Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Rwanda ifikapo mwaka 2014 itakuwa inafikia ukomo wake kadiri ya taratibu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa. Licha ya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, Jumuiya ya Kimataifa imejifunza mambo mengi kutoka Rwanda kwamba, watu wanapaswa kuwa makini na uchochezi na chuki za kikabila zinazopigiwa debe mara nyingi na vyombo vya habari kwa mafao yao binafsi.

Rwanda imeweza kuimarisha mfumo wa mahakama za kitaifa zinazojulikana kama Gachacha, hapa ni mahali ambapo washitakiwa walipewa nafasi ya kuweza kutubu na kuomba msamaha kutokana na makosa waliyoitendea Jamii, wakiahidi kuanza upya kwa kuwa watu wema zaidi. Jumla ya mahakama 12, 000 za Gachacha zilianzishwa nchini Rwanda na kusikiliza kesi za watu zaidi ya millioni moja nukta mbili.

Mahakama hizi zilisaidia kwa namna ya pekee katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa kwani watu waliambiwa ukweli kuhusu mauaji ya ndugu zao. Baada ya kumaliza kazi zake, zilifungwa rasmi hapo tarehe 4 Mei 2012.

Umoja, upatanisho na mshikamano wa kitaifa ni kati ya vipaumbele vilivyoanza kufanyiwa kazi na Rwanda mara baada ya mauaji ya kimbari. Lengo ni kuhakikisha kwamba, haki inatendeka, watu wanafahamu ukweli wa mambo na hatimaye wanaanza kujenga, kudumisha na kuimarisha misingi ya: usalama, amani na utulivu.

Rwanda inatambua na kuheshimu kwamba, raia wake wote ni sawa mbele ya sheria na wana haki sawa! Hapa sheria zinalenga kuondoa chembechembe za ubaguzi na utengano zilizopelekea hata kuibuka kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Jumuiya ya Kimataifa ikashangaa kwa unyama ambao binadamu angeweza kutenda katika maisha yake!

Umoja wa Mataifa unasema kwamba, kati ya vipaumbele vinavyopewa nafasi ya kwanza nchini Rwanda kwa sasa ni Umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na upatanisho unaoendeshwa na Tume ya Upatanisho iliyoundwa kunako mwaka 1999. Tume hii ina majukumu ya kuhamasisha misingi ya haki na amani, kazi iliyoanza kunako mwaka 1999 hadi mwaka 2009 na wananchi laki tisa waliweza kufaidika na mafunzo ya haki na amani yaliyokuwa yanatolewa nchini Rwanda katika mfumo unaojulikana kama "Ingando".

Wananchi wamefundishwa na kujulishwa kuhusu chembechembe za ubaguzi, migawanyo kati ya watu na wakawezeshwa kujenga na kuimarisha uzalendo, umoja na mshikamano wa kitaifa, mambo ambyo ni msingi mkubwa wa amani na utulivu.

Kunako mwaka 2007 Rwanda ilizindua Programu ya mafunzo ya Uongozi wa umma yanayojulikana kama "Itorero". Hapa Rwanda ilitoa mafunzo kuhusu tunu msingi za maisha ya kijamii kwa ajili ya viongozi wa kijamii, watakaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Rwanda katika ujumla wao bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile! Kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2009, jumla ya wananchi 115, 228 walishiriki.

Pamoja na mikakati iliyobainishwa hapo awali, Rwanda tangu mwaka 2000, imekuwa ikiendesha semina za kitaifa ili kuzungumzia mada nyeti kama vile: haki, utawala bora, haki msingi za binadamu; usalama wa taifa na historia ya wananchi wa Rwanda. Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda yamefuatiliwa pia kisayansi kwa kufanya tafiti za kina na mapana ili kubaini vyanzo vya chokochoko za kikabila na jinsi ya kuzidhibiti kwa ajili ya mafao ya wengi sanjari na kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.