Wakora Ta Nestor Timanywa, karibu Askofu Rwoma Jimboni Bukoba!
Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro anamshukuru na kumpongeza Askofu
mstaafu Nestor Timanywa wa Jimbo Katoliki Bukoba kwa kazi kubwa ya kitume aliyoifanya
kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Bukoba, Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania na kwa watanzania wote waliobahatika kupata huduma yake
kama Askofu.
Katika mahojiano
maalum na Radio Vatican, Askofu Mkude anakiri kwamba, kunako mwaka 1975 walipokutana
kwa mara ya kwanza, alishangaa kumwona Askofu kijana kabisa katika maisha yake na
Askofu Timanywa alimwomba ili aweze kumwombea kwa Mungu amsaidie katika maisha na
utume wake kama Askofu.
Ni kiongozi ambaye ameonesha unyofu, utaratibu na
kwamba, Askofu Timanywa kwa hakika ni mtu wa watu. Kanisa linamshukuru na kumpongeza
kwa utume wake na kwa sasa anastahili kupumzika ili aweze kupata muda zaidi wa kusali
na kutafakari kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa Jimboni Bukoba.
Askofu
Mkude anasema, wanafahamiana vizuri na Askofu Rwoma wa Jimbo katoliki Bukoba na Msimamizi
wa kitume wa Jimbo Katoliki Singida. Askofu Rwoma ambaye enzi zake alikuwa ni mchezaji
mahiri wa mpira wa miguu, sasa kwa unyenyekevu mkubwa amejiweka kuwa ni mpira wa Mungu.
Anampongeza kwa kuteuliwa kuliongoza Jimbo Katoliki Bukoba ambalo ni kubwa
na lina waamini na changamoto nyingi, ikilinganishwa na Jimbo Katoliki Singida. Jambo
la msingi ni kujipa moyo, kila jambo linawezekana kwa mtu mwenye imani thabiti, bidii
na utashi wa kusonga mbele kwa kasi na ari kubwa zaidi.
Askofu Mkude anawaalika
Watu wa Mungu Jimbo Katoliki Bukoba, kutoa ushirikiano mkubwa kwa Askofu Rwoma, kwani
ni mtu mwenye mipango, jasiri na Mchamungu. Ameteuliwa kwa kazi maalum na kwa wakati
maalum kwa ajili ya Jimbo Katoliki Bukoba.