Viongozi wa kitaifa, wekeni bayana sera na mikakati ya kupambana na baa la njaa nchini
mwenu!
Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja
wa Mataifa, FAO, amewataka viongozi wa kitaifa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza wajibu
wao msingi, ili watu wao waweze kuwa na uhakika na usalama wa chakula mara baada ya
kuhitimisha mikakati ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia hapo mwaka 2015. Serikali
zinapaswa kujipanga kikamilifu ili kupambana na baa la njaa ambalo bado limekuwa ni
tishio kwa maisha ya watu wengi duniani.
hadi sasa kuna dalili za maendeleo
yaliyokwishafikiwa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia, lakini
bado kuna watu zaidi ya millioni 870 wanaokabiliwa na baa la njaa. Mikakati ya kuwa
na uhakika wa usalama wa chakula bado haijapata mafanikio ya kutosha, kumbe kuna haja
kwa viongozi wa Kitaifa kujipanga vyema ili kukabiliana na changamoto hii, kwa kutambua
kwamba, chakula ni sehemu ya haki msingi za binadamu, jambo linalohitaji sera makini
kwa siku za usoni.
Bwana Josè Graziano da Silva ameyasema hayo siku ya Alhamisi
tarehe 4 Aprili 2013 alipokuwa anazungumza na wajumbe wa ngazi za juu uliokuwa unajadili
taswira ya Umoja wa Mataifa baada ya Mwaka 2015. Anasema, Jumuiya ya Kimataifa ina
uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha kwa watu wengi, kumbe, jambo la msingi kwa
wakati huu ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na maboresho ya lishe katika ngazi za
vijijini.
Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na uwekezaji katika shughuli
za kilimo na uzalishaji vijijini, mahali ambapo asilimia 70 ya watu wanaokabiliwa
na njaa wanaishi; sehemu ambako wananchi wengi wanategemea kilimo kwa ajili ya maisha
yao kwa kutoa ajira ya watu zaidi ya millioni 500. Mkakati huu hauna budi kuungwa
mkono na sera makini za uchumi wa dunia; amani na utulivu, kwani kinzani na migogoro
imepelekea kushuka kwa uzalishaji katika sekta ya kilimo.
Kuna haja pia ya
kulinda na kutunza mazingira pamoja na rasilimali za nchi. Juhudi hizi zinapaswa kutekelezwa
kwa mshikamano wa dhati kati ya nchi husika na Jumuiya ya Kimataifa.