Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Huruma ya Mungu
Katika furaha ya Pasaka, tunaendelea kuzitangaza sifa za Bwana kwa mataifa yote, tukiwa
tayari Dominika ya II ya Pasaka mwaka C. Neno la Mungu linatufundisha kuitazama Jumuiya
ya Kwanza iliyohuishwa na Neno la Mungu kama hakiki ya kwamba Yesu Kristu amefufuka
na anaishi.
Mwinjili Yohane
anakazia Imani, zaidi ya kuona, Bwana akisema wa heri wanaosadiki bila kuona. Mwinjili
anasonga mbele akiweka mbele yetu ungamo la imani la Mtakatifu Thoma Mtume ambaye
mwanzoni alionesha hali ya kutokuamini mpaka awe amegusa makovu ya Bwana!
Bwana
akishawatokea Mitume waliokuwa wamekusanyika pamoja na kuwatakia amani ambalo ni tunda
la ufufuko atawavuvia Roho Mtakatifu ili wapate kuondolea dhambi, wapate kukabiliana
na nguvu za giza. Ni katika siku hii Yesu Kristo mfufuka anaweka sakramenti ya Kitubio.
Jambo moja la kukumbuka katika siku zetu hizi ni kujua kuwa, Roho Mtakatifu
ni amani na wala si ugomvi na vurugu katika maisha yetu. Tuwe makini na shughuli mbalimbali
amabazo hufanywa katika madai yakwamba tumetumwa na Roho Mtakatifu. Ni lazima nyuma
yake kutanguliwe na amani na kisha kumalizike na amani.
Mpendwa mwana pasaka
Bwana anawatokea mitume wakiwa wamekusanyika katika jumuiya na anawapatia salamu yake
maarufu sana yaani “amani iwe kwenu”. Mara moja Bwana anataka kusisitiza maisha ya
jumuiya na hivi ni katika jumuiya twaweza kusikia na kusikiliza Neno na salaamu ya
Mwenyezi Mungu. Ni kwa jinsi hiyo basi asiyekuwepo katika jumuiya hawezi kuipata salaamu
hiyo na kusikia Neno la Mungu.
Bwana anapotoa salaam hiyo anaifungamanisha
na furaha, Roho Mtakatifu na amani kumbe jumuiya ni kitovu cha Roho Mtakatifu na amani.
Leo hii tunazo jumuiya ndogondogo, tunalo kusanyiko la Ekaristi Takatifu Dominika
na siku nyingine, tuanayo mikutano ya Halmashauri, kwaya hivi vyote ni nafasi mwanana
kwa ajili ya kupokea neema za Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu, kumbe yafaa tuviadhimishe
kwa ustadi na upendp mkubwa.
Mtume Thoma ambaye anataka kuona ndipo aamini
ni kielelezo cha mateso na hofu ya Mitume kabla ya kuamini ufufuko wa Bwana. Kwa hakika
haikuwa rahisi kwa Mitume kuamini pamoja na matokeo ya mbalimbali ya Bwana lakini
polepole watafikia kilele cha imani. Katika hili Mwinjili anataka kuwasaidia waamini
ambao walipenda kuona kabla ya kuamini, kwamba Kristu mfufuka hafungwi na milango
ya ufahamu bali anaonekana kwa imani.
Na kwa hakika imani haipatikani katika
kile tunachokiona, kumbe anayetaka kugusa na kuona hawezi kuwa na imani. HERI WASIOONA
NA WAKAAMINI. Tena haya yameandikwa ili tuweze kusadiki na kuamini, na kwa namna hiyo
hakuna njia nyingine ya kusadiki isipokuwa kwa njia ya NENO LA MUNGU. Kondoo wangu
huijua sauti yangu,Yn 10:14,17 na hivi sauti ya Kristu husikika katika Injili yake.
Katika
somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume tunapata maelezo ya maisha
ya Jumuiya ya kwanza huko Yerusalemu, jumuiya ambayo chimbuko lake ni Imani katika
Yesu mfufufka. Kwa sababu ya imani waliyoipokea Mitume na kuiishi, Jumuiya ya Waamini
ilizidi kuongezeka. Mitume waliwaponya watu shida zao mbalimbali, waliwahubiria Neno
la Mungu na hili lilitokana na uhakika wao kwamba Bwana anaishi. Waamini waliongezeka
kwa sababu Mitume walifanya alichofanya Bwana, nasi hivi tunaalikwa kufanya kilekile
alichofanya Bwana.
Mpendwa mwana wa Mungu katika somo la pili katika kitabu
cha ufunuo tunakutana na Mt. Yohane ambaye yuko katika kisiwa cha Patimo. Yuko huko
kwa sababu ya imani yake katika Kristu mfufuka. Yuko uhamishoni, ni wakati wa Domisiani
aliyetaka kuabudiwa kama Mungu na hivi Yohane anakataa! Mt. Yohane anataka kuwaimarisha
wanaoteseka kwa sababu ya madhulumu wavumilie mateso yao wakitarajia furaha iliyo
kuu yaani uzima wa milele.
Anatumia alama mbalimbali ambazo zataka kuleta
ujumbe kwa waamini wanaoteswa. Ipo alama ya mwanadamu kati ya vinara 7, huyu ni Kristu
mfufuka, vazi refu ni alama ya kuhani ambaye kwa sasa ni Kristo na wala hakuna mwingine,
na hivi tumfuate yeye. Mshipi ambao amejifunga ni alama ya kifalme.
Mpendwa
jambo ambalo Mt. Yohane ataka kulijenga ni kuwa Kristu mfufuka ndiye kitovu na dira
ya maisha yetu, kumbe kila mmoja wetu ataweza kufika mbingu akipita kwa Bwana.
Nikutakie
maisha ya Pasaka yaliyo ya furaha na zaidi tukikomaza Jumuiya Ndogondogo ambazo kwazo
Kristo uhubiri Neno kila siku mpaka ukamilifu wa dahari. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C.PP.S.