Hija ya imani kuelekea Maadhimisho ya Siku ya 8 ya Familia Kimataifa, huko Philadelphia
2015
Kengele ya uhuru ni alama muhimu sana kwa Jiji la Philadelphia, Marekani, ambalo litakuwa
ni mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa, itakayofanyika kuanzia
tarehe 22 hadi 27 Septemba 2015. Hii ni kengele iliyopigwa kwa mara ya kwanza kunako
mwaka 1779 kuwaalika wananchi wa Marekani kukusanyika pamoja ili kusomewa tamko la
uhuru wa Marekani.
Nembo ya Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa
inaonesha kengele ambayo iko kati kati na kuzungukwa na nyota, ili kuonesha umuhimu
wa Jiji la Pennsylvania lililosimama kidete kulinda na kutetea haki za kijamii na
uhuru wa kidini. Kwa upande wa Kanisa, kengele inagongwa ili kutangaza Habari Njema
ya Familia kwa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaoalikwa kwa namna ya pekee,
kushiriki katika maadhimisho ya Familia Kimataifa yatakayofanyika nchini Marekani
kwa Mwaka 2015.
Katikati ya Nembo kuna Msalaba unaomwonesha Kristo kuwa ni
kiini cha Maadhimisho na maisha ya waamini. Inawaonesha watu watano wenye maumbo na
umri tofauti; kielelezo cha dhamana zinazotekelezwa na wanafamilia katika hali ya
umoja na mshikamano: hawa ni wazazi, watoto, ndugu na jamaa. Baraza la Kipapa la Familia
limetumia fursa hii pia kuzindua tovuti itakayokuwa na mambo mbali mbali kuhusiana
na Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa kwa Mwaka 2015, itakayofanyika
Jijini Philadelphia.
Unaweza kupata habari zaidi kwa kutumia anuani ifuatayo:
www.worldmeeting2015.org
Askofu
mkuu Charles Chaput wa Jimbo kuu la Philadelphia ambaye atakuwa ni mwenyeji wa Maadhimisho
haya anasema, Jimbo lake, utakuwa ni mji wa kwanza kabisa nchini Marekani kuweza kuwa
ni mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa, iliyoanzishwa na Mwenyeheri
Yohane Paulo wa pili, kunako mwaka 1994.
Lengo ni kuimarisha tunu msingi na
maisha ya kifamilia. tangu wakati huo, Kanisa limeendelea kutafakari tunu msingi za
maisha ya kifamilia, fursa, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika hija
ya maisha yao ya kila siku.
Viongozi wa serikali kutoka Pennsylvania tangu
wakati huu, wanazikaribisha kwa mikono miwili, familia kutoka sehemu mbali mbali za
dunia Jijini humo. Ni matumaini ya viongozi hawa kwamba, Maadhimisho ya Nane ya Familia
Kimataifa, litakuwa ni tukio kubwa linalotarajiwa kuacha chapa ya kudumu katika maisha
ya waamini na wananchi kwa ujumla wao.