2013-04-05 10:17:24

Amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu


Amani si bidhaa inayoweza kuuzwa na kununuliwa dukani, bali ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu. Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae, Alhamisi, tarehe 4 Aprili 2013.

Anasema, wafuasi wa Yesu waliokuwa wanakwenda Emmaus walishangazwa na muujiza wa Yesu alipoumega mkate na hatimaye akatoweka mbele yao. Baba Mtakatifu alikuwa anafanya tafakari ya Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Luka: 24: 35 - 48.

Mitume wa Yesu walipigwa na bumbuwazi walipomwona na kumsikia Yesu akizungumza na kula pamoja nao! walijazwa na furaha ya ajabu, kiasi cha kudhani kwamba wamepagawa anasema Baba Mtakatifu Francisko! Hii ni furaha inayopata chimbuko lake pale mwamini anapokutana na Yesu katika hija ya maisha yake, tukio ambalo linaacha alama ya kudumu katika moyo na maisha ya mwanadamu.

Hali hii inapaswa kuleta faraja kwa waamini hata kama wanakabiliana na hali ngumu katika maisha yao, kwani hii ndiyo ile amani ya ndani ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na uwapo endelevu wa Yesu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anawachangamotisha waamini kuwa na ujasiri wa kuomba neema hii katika maisha yao; yaani neema ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao. Ni mwaliko kwa waamini kudumisha amani na utulivu wa ndani, kwa kumtafakari Kristo ambaye aliteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, kamwe hakupoteza amani, zawadi ambayo anapenda kuwashirikisha wafuasi wake.

Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na wafanyakazi kadhaa wa Vatican. Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake kwa kuwataka waamini kuendelea kusali kwa ajili ya kuomba kupata: neema, faraja na kitulizo kwa kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao. Misa zinazoendeshwa na Baba Mtakatifu kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae ni nafasi kwake kuweza kukutana, kuzungumza na hatimaye kufahamiana na wafanyakazi wa Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.