Ratiba elekezi za Ibada zitakazoadhimishwa na Papa Francisko mwezi Aprili-Mei 2013
Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa Monsinyo Guido Marini, ametoa ratiba elekezi
ya Ibada zinazotarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Mwezi
Aprili hadi Mwezi Mei, 2013.
Tarehe 7 Aprili 2013, Jumapili ya Pili ya Kipindi
cha Pasaka, maarufu pia kama Jumapili ya Huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko,
Saa 11:30 Jioni, atasimikwa rasmi kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma katika Ibada
ya Misa Takatifu itakayofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano,
Makao Makuu ya Jimbo kuu la Roma.
Tarehe14 Aprili 2013, Jumapili ya Tatu ya
Kipindi cha Pasaka, Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye
Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma, kuanzia Saa 11:30 Jioni.
Tarehe
21 Aprili 2013, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo
Mchungaji mwema, Siku ya 50 ya Kuombea miito iliyoanzishwa na Papa Paulo wa sita na
kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu "Miito mitakatifu ni alama ya matumaini yanayosimikwa
katika imani. Hii itakuwa ni fursa muhimu kwa Baba Mtakatifu Francisko kutoa Sakramenti
ya Daraja Takatifu kwa Mashemasi walioandaliwa tayari. Ibada ya Misa ya Upadrisho
inatarajiwa kuanza saa 3:30 asubuhi.
Tarehe 28 Aprili 2013, Jumapili ya tano
ya Kipindi cha Pasaka, Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada ya Misa takatifu
na kutoa Sakramenti ya Kipaimara. Na kwa kuwaimaarisha Wakristo katika Sakramenti
ya Kipaimara ili wawe tayari kutolea ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake, Baba
Mtakatifu Francisko atakuwa anakunja jamvi la Maadhimisho ya Ibada kwa Mwezi Aprili,
2013.
Mwezi Mei, ambao kadiri ya Mapoke ya Kanisa umetengwa rasmi kwa ajili
ya Ibada kwa Bikira Maria, Baba Mtakatifu Francisko atakuwa na majukumu kadhaa ya
kutekeleza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Tarehe
4 Mei 2012, Jumamosi, majira ya saa 12:00 jioni, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa
kuungana na waamini watakaokuwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu lililopo mjini
Roma kwa ajili ya kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa Injili.
Tarehe 5 Mei
2013, Jumapili ya Sita ya Kipindi cha Pasaka, Baba Mtakatifu Francisko ataungana na
mashirika mbali mbali kwa ajili ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4:00 asubuhi.
Tarehe 12 Mei
2013, Jumapili ya Saba ya Kipindi cha Pasaka, Baba Mtakatifu Francisko majira ya saa
3:30 asubuhi anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwatangaza
wenyeheri: Antonio Primaldo na wenzake; Laura wa Mtakatifu Katerina wa Siena na Maria
Guadalupe Garcìa Zavala kuwa Watakatifu.
Tarehe 18 Mei 2013, Kesha la Pentekoste,
Saa 12:00 Jioni, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba
Mtakatifu Francisko atafanya Kesha la Siku kuu ya Pentekoste, kuzaliwa kwa Kanisa
na Siku ya Waamini Walei duniani, wanapotumwa kwenda ulimwenguni kwa ajili ya kuyatakatifuza
malimwengu na Vyama vya Kitume.
Tarehe 19 Mei 2013, Siku kuu ya Pentekoste,
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, m ajira ya saa 4:00 asubuhi, Baba
Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na wanachama wa mashirika na
vyama vya kitume. Kwa ufupi, hii ndiyo ratiba elekezi iliyotolewa na Monsinyo Guido
Marini, Mshehereshaji mkuu wa Ibada za Kipapa. Kama ilivyo ada, Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican, itaendelea kukujuza yale yatakayojiri kutoka katika Ibada hizi.
Unaweza pia kufuatilia matukio haya kwa njia ya mtandao wa Radio Vatican kwa anuani
ifuatayo: