Changamoto za Uinjilishaji Mpya mintarafu mchango wa Kardinali Jorge Mario Bergoglio
Kardinali Jaime Lucas Ortega Alamino, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Havana, Cuba, akishirikisha
mang’amuzi yake kutokana na mikutano elekezi iliyofanywa na Makardinali wakati wa
mchakato wa kumchagua Papa Mpya anabainisha kwamba, tafakari iliyotolewa na Kardinali
Jorge Mario Bergoglio ilikuwa wazi na dira muhimu sana kwa Mama Kanisa katika mchakato
wa Uinjilishaji Mpya, changamoto inayovaliwa njuga wakati huu. Anasema, alishiriki
kikamilifu katika kumuaga Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliyeng’atuka
kutoka katika uongozi ili kupata muda zaidi wa kusali na kutafakari kwa ajili ya mafao
na ustawi wa Kanisa la Kristo. Kardinali Bergoglio alitoa changamoto ya kina kuhusu
maisha na utume wa Kanisa mintarafu changamoto za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Kardinali Ortega anasema, aliposikiliza tafakari hii, alikwenda moja kwa moja
kwa Kardinali Bergoglio ili kuomba karatasi ya tafakari yake naye bila uchoyo wala
roho ya kwanini, akampatia kikaratasi kilichokuwa kimeandikwa kwa mkono, kuonesha
mawazo yake makuu katika mkutano elekezi kwa Makardinali wakati wa mchakato wa kumchagua
Papa Mpya. Kardinali Bergoglio alipochaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro,
kwa mara nyingine tena Kardinali Ortega alimwomba ruhusa ya kutumia mawazo yake kwa
ajili ya kuwashirikisha waamini wake wakati huu Kanisa linapoendeleza mchakato wa
Uinjilishaji Mpya. Kardinali Bergoglio katika hotuba yake kwenye mkutano wa Makardinali,
alikazia mambo makuu manne: Uinjilishaji; Kanisa kujikosoa; Kanisa kutoka ndani mwake
ili kwenda kuinjilisha pamoja na kumruhusu Kristo kutoka ndani mwao ili kuwaendea
wote wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kuhusu mchakato wa Uinjilishaji
Mpya, Kardinali Bergoglio wakati huo aliwachangamotisha Makardinali kwa kuwaambia
kwamba, Kanisa halina budi kutoka ndani mwake, ili kuwaendelea wale wanaoishi pembezoni
mwa Jamii, waliokata tama ya maisha; wanaokabiliana na hali ngumu kutokana uwepo wa
dhambi, ukosefu wa haki msingi za binadamu, magonjwa, njaa na ujinga. Kanisa halina
budi kujitoa kimasomaso kwa ajili ya Uinjilishaji badala ya kujitafuta lenyewe, kiasi
cha kulitenga na kile kinachoendelea ulimwenguni. Ni mwaliko wa kwenda ulimwenguni
ili kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha amini na adili. Kwa njia
hii, Kanisa linaweza kumruhusu Kristo kutoka ndani mwao na kuwagusa wale wanaohitaji
kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka. Kanisa linalojiinjilisha, linapaswa
kuwa ni mwanga na chumvi ya dunia, ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa ndani ya Kanisa.
Mwishoni, Kardinali Bergoglio aliwaasa Makardinali wenzake wawe ni watu wa sala na
tafakari ya kina kuhusu Kristo, ili hatimaye, aweze kuwasaidia katika kutekeleza utume
wao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Anasema, kwa namna ya pekee, Kanisa
linatumwa kuwaendelea wale wanaoishi pembezoni mwa Jamii: kiroho na kimwili. Hii ni
changamoto kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Kanisa linawahitaji
watu wanaosali na kufanya tafakari ya kina kuhusu Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka.
Viongozi, wawe waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, hii ndiyo ile furaha ya Uinjilishaji
Mpya!