2013-04-03 12:09:07

Yanayomkabili Rais Uhuru Kenyatta baada ushindi wake!


Ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta na Mgombea mwenza William Ruto wanaotarajiwa kuapishwa hapo tarehe 9 Aprili 2013 kuongoza Kenya ni kielelezo tosha kwamba, Kenya imejifunza kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyotokea kunako mwaka 2007 na kupelekea watu zaidi ya 1,000 kupoteza maisha na wengine kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa na haki msingi za binadamu wanaendelea kufuatilia kwa karibu zaidi tuhuma dhidi ya viongozi hawa wakuu wa Serikali ya Kenya wanaopaswa kufikishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ili kujibu tuhuma za mauaji zinazowakabili. Mwendesha mashtaka wa Mahakama hii Fatou Bensouda amedhamiria kuendeleza kesi hii kadiri ilivyopangwa kusikilizwa mwezi Mei kwa William Ruto na Mwezi Julai kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Huu utakuwa ni mtihani mgumu kuweza kupatiwa ufumbuzi kwani nchi nyingi zimeonesha kutoridhika na mwenendo wa kesi katika mahakama hii kwani zinaonekana kuwa zinaelemea upande mmoja, yaani wananchi na viongozi wanaotoka katika nchi zinazoendelea duniani wakati ambapo "vigogo wa vita" wanaendelea kutanua mitaani!

Rais Uhuru Kenyatta anakabiliwa pia na mtihani wa uhusiano wa kidiplomasia na nchi nyingi za Magharibi ambazo zilitoa tahadhari kuhusu kuchaguliwa kwake kuwaongoza wananchi wa Kenya.







All the contents on this site are copyrighted ©.