2013-04-03 08:22:42

Waamini wanahamasishwa kujitosa kimaso maso katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia baada ya maadhimisho ya mkutano wake wa kumi, uliofanyika hivi karibuni nchini Vietnam na kuhudhuriwa na Kardinali Gaudencio Rosales, mwakilishi maalum wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita pamoja na Askofu mkuu Savio Hon Tai Fai, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. RealAudioMP3

Jumla ya wajumbe mia moja na kumi na mmoja walishiriki katika tukio hili la kihistoria, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka arobaini tangu Katiba ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Asia, lilipoidhinishwa kwa mara ya kwanza.

Maadhimisho haya yamekwenda sanjari na Mwaka wa Imani, Kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 ya Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, bila kusahau Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya iliyofanyika mjini Vatican kwa kutoa changamoto ya kumshuhudia Kristo kwa ari na moyo mkuu zaidi bila ya kukatishwa tamaa. Wajumbe walionja umoja na mshikamano wa Kanisa Barani Asia, ingawa walisikitika kukosa wawakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki China.

Maaskofu wanawashukuru watawa na waamini walei wanaoendelea kujitoa kwa hali na mali katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu Barani Asia, licha ya vitisho na hali ngumu wanayokabiliana nayo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Kanisa linatambua kwamba, kwa sasa halina budi kujikita kujifungamanisha na Kristo ili kwa pamoja kama Jumuiya, liweze kumshuhudia Kristo kwa maneno, lakini kwa njia ya matendo yao adili.

Kanisa Barani Asia, likiwa linasukumwa na ari na moyo wa kimissionari uliotangazwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, watambue dhamana na utume wao wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwani kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wamekuwa ni wadau wa Uinjilishaji, wanaotumwa sehemu mbali mbali za dunia kuyatakatifuza malimwengu na kuwashirikisha wengine ile furaha ya kukutana na Kristo katika hija ya maisha yao ya Kiimani hapa duniani. Ni hija inayojikita katika toba na wongofu wa ndani, ikashuhudiwa katika imani tendaji inayojionesha kwa namna ya pekee katika matendo.

Historia ya maisha na utume wa Kanisa Barani Asia inafumbata utume na ushuhuda uliotolewa na wafiadini, waliothubutu kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, leo hii, damu yao imeendelea kuwa ni chemchemi ya Ukristo Barani Ulaya. Hawa ni watawa na waamini walei waliwajibishwa na upendo wa Kristo, kiasi kwamba, hawakuona tena maisha yao kuwa ni kitu cha kung’angania sana, bali kuyatoa sadaka kwa ajili ya sifa na utukufu wa Kristo.

Kanisa Barani Asia, linatumwa kujenga Ufalme wa Mungu unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kiasi kwamba, imani inajionesha katika matendo na vipaumbele vya waamini katika medani mbali mbali za maisha yao. Ni mwaliko wa kuweka tunu msingi za maisha na kweli za Kiinjili katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu.

Ni mwaliko wa kuendelea kujenga mshikamano wa umoja na upendo, wakichota mfano na kielelezo kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu; tayari kujimwaga ulimwenguni kwa ajili ya utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji, kama Familia ya Mungu, licha ya dhuluma, vitisho na magumu wanayokabiliana nayo Barani Asia. Waamini wajenge na kuimarisha Umoja na mshikamano unaojionesha katika: Familia, Parokia, Majimbo na Kanisa na Kiulimwengu.

Kanisa Barani Asia linawajibika kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa wafuasi wa Kristo na waamini wa dini mbali mbali kama njia ya Uinjilishaji Mpya unaojionesha katika huduma makini kwa Jamii, ili watu watambue na kuonja uwepo wa Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Maskini, wagonjwa, wazee na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii wapewe kipaumbele cha kwanza katika utume na maisha ya Kanisa. Waamini wajenge ndani mwao moyo wa Ibada, Tafakari ya kina na Ukimya, ili kutangaza upendo wa Mungu unaokoa, kwa kujikita katika kulinda na kutetea haki msingi za binadamu.

Waamini Barani Asia wanachangamotishwa kuonesha mshikamano wao wa dhati kwa wote wanaonyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; wanaoendelea kuathirika kwa mashamulizi ya kigaidi na misimamo mikali ya kiimani bila kuwasahau wanaotengwa kwa sababu ya mila na desturi zilizopitwa na wakati.

Ni wajibu wa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutunza mazingira kama mwendelezo wa kazi ya uumbaji, kwani katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, ubinafsi na uharibifu wa mazingira umepelekea athari kubwa zinazojionesha katika mabadiliko ya tabia ya nchi na madhara yake katika maisha ya watu wengi Barani Asia.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia linabainisha kuwa, matukio mbali mbali yanayoadhimishwa na Mama Kanisa katika Mwaka wa Imani, yawe ni chachu ya kuleta mwamko, ari, kasi na nguvu mpya miongoni mwa wakristo katika kutangaza Injili ya Kristo; kwa kukazia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia za Kikristo; umoja na mshikamano wa dhati; toba na wongofu wa ndani ili kuchuchumilia utakatifu wa maisha kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda amini wa imani tendaji.

Hakuna sababu ya kuogopa kwani Kristo amewahakikishia wafuasi wake, uwepo wake wa daima hadi utimilifu wa dahali. Hivi ndivyo Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Asia, linavyohitimisha Ujumbe wake mara baada ya Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa kumi, uliofanyika hivi karibuni, sanjari na kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu Shirikisho hili lilipoanzishwa Barani Asia.








All the contents on this site are copyrighted ©.