Umuhimu wa hija za maisha ya kiroho katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani
Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliozinduliwa
na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita sanjari na Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka
50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 ya Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki,
muhtsari wa Mafundisho Tanzu ya Kanisa, waamini nchini Nigeria wanaalikwa kwa namna
ya pekee kushiriki katika hija za maisha ya kiroho zilizopangwa na Parokia, Majimbo
na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria. Hija hizi zinaendelea kufanyika mjini
Roma ambako kuna utajiri mkubwa wa ushuhuda wa imani na katika Nchi Takatifu, mahali
ambako Yesu alitekeleza utume wake wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa
dhambi na mauti. Ili waamini waweze kujipatia rehema kamili zinazotolewa na Mama Kanisa
katika hija za maisha ya kiroho, wanapaswa kujiandaa kikamilifu kwa kutimiza masharti
yote yanayotolewa na Kanisa pamoja na kujiandaa vyema katika maisha ya kiroho.
Waamini
wanahamasishwa zaidi kwa kufanya toba na kushiriki kwa ufahamu zaidi wa Mafumbo ya
Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria limepanga hija tatu za maisha ya kiroho
katika maeneo matakatifu. Kati ya hija hizi, moja ni maalum kabisa kwa ajili ya Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani. Hija ya kwanza ni ile ambayo imepangwa kwa ajili ya Juma kuu
na ilianza tarehe 25 Machi hadi tarehe 1 Aprili 2013. Waamini watapata fursa ya kutembelea
San Giovani Rotondo, Lanciano na Roma. Waamini, wakaadhimisha Fumbo la Pasaka na Papa
Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii ni bahati
iliyowangukia wale ambao wameshiriki katika kundi la kwanza katika Maadhimisho ya
Mwaka wa Imani. Kundi la Pili litaanza hija yake tarehe 8 hadi 19 Mei 2013. Hawa
watatembelea Israeli, Roma, Cascia na Assisi. Lengo ni kuwawezesha Waamini kuadhimisha
Siku kuu ya Pentekoste pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakiwa imara katika imani,
matumaini na mapendo, waweze kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake,
katika maisha na vipaumbele vyao. Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linasema
kwamba, Kundi la tatu la mahujaji kutoka nchini humo litaanza hija yake tarehe 25
hadi 30 Septemba 2013. Hii ni nafasi ya pekee kwa Makatekista ambao ni wadau wakuu
wa Uinjilishaji Barani Afrika kupata nafasi ya kukutana na Katekista Mkuu, Khalifa
wa Mtakatifu Petro. Maaskofu wanawaomba waamini katika Parokia na Majimbo yao kuwawezesha
Makatekista kwa hali na mali ili kushiriki katika hija hii ya maisha ya kiroho, kama
sehemu ya mchakato wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Huu ni wakati wa Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani kwa Makatekista kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watakaokusanyika
hapa mjini Roma kwa wakati huo. Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linabainisha
kwamba, hija nyingine mbili zilizopangwa katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani zitafanywa
mjini Roma, Lourdes, Ufaransa na Fatima, Ureno. Kwa waamini watakaokwenda Fatima,
watashiriki pia kumbu kumbu ya miaka 96 tangu Bikira Maria wa Fatima alipowatokea
wale watoto watatu wa Fatima, yaani Francis, Yacinta na Lucia.
Hija hii itafanyika
kuanzia tarehe 8 hadi 9 Oktoba 2013, ili kuwawezesha waamini kushiriki pia katika
Sherehe za Kuufunga Mwaka wa Imani, changamoto na mwaliko kwa waamini kutolea ushuhuda
wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, si tu kwa maneno, bali kwa njia ya matendo
yao!