Tume ya haki na amani Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: tujenge kwa pamoja Tanzania
yenye haki na amani!
Mkutano wa kitaifa wa wajumbe wa Tume ya Haki na Amani za majimbo ya Kanisa Katoliki
Tanzania na Wanataaluma Wakristo Tanzania (CPT) ulifanyika kwenye Kituo cha Kiroho
cha Mbagala tarehe 26-27 Februari, 2013. Wakitafakari na
kutaamuli juu ya hali ya maisha nchini na uwajibikaji wa kila mmoja wetu katika kutunza
na kujenga haki na amani nchini mwetu, wameonesha kusikitishwa sana na hata kuingiwa
hofu na mashaka kwa matukio ya kihalifu na mienendo isiyo ya kawaida inayojidhihirisha
nchini nyakati hizi. Waliogopeshwa na kuenea kwa uchoyo na fikra-potofu zinazojidhihirisha
kwa misimamo na mihadhara ya kiimani kali na kilokole, ambayo hupotosha ukweli halisi
wa dini iliyo na wajibu mkuu wa kulea urafiki na mapatano miongoni mwa watu. Waliona
kuwa ni wajibu wa kila mmoja wetu na wa kila mamlaka ya uongozi wa kijamii na wa kiroho,
kujihusisha kwa vitendo thabiti katika ujenzi wa amani na kukubali pasipo shaka yoyote
utofauti wetu kuwa ni baraka na chemchemi ya vipaji na rasilimali mbalimbali zitakiwazo
katika kila medani za maisha ya taifa na siyo chanzo kisichovumilika cha kukataana
na kuhasimiana. Tunawasihi viongozi wetu wa serikali zote mbili kutoruhusu mashambulio
ya aina yoyote kwa watu wa imani mbalimbali, uchomaji wa makanisa, kashfa dhidi ya
misahafu na vitabu vitakatifu vya imani tofauti za Watanzania. Tumeona vikundi vya
watu mahususi vikiachiwa kuzunguka nchini kote huku vikishambulia waamini wa dini
tofauti na ya kwao kwa jeuri bila ya hofu ya sheria wakati Katiba ikizitaka serikali
zote mbili na vyombo vya ulinzi kuondoa aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa,
uonevu au upendeleo. Vyombo vya ulinzi sharti vitekeleze wajibu wao na kutoruhusu
uwepo wa vikundi hivyo na mienendo ya imani na itikadi kali. Tunatambua kwamba
dini inatumika kwa ajenda ya kisiasa ya kulazimisha dini moja juu ya jamii inayojulikana
kufuata dini mbalimbali. Vikundi halifu hivyo vinaikashifu dini wanayoitumia kisiasa
kwa madhumuni ya kutwaa utawala wa nchi. Wakati huu ambao taifa limo katika zoezi
la kuandika Katiba mpya, vikundi hivi vidogo vya kichochezi vinaweza kabisa kusambaratisha
mchakato huo. Hali hii inasikitisha sana kwani imesababisha uhai kutoweka kwa mauaji
ya wazi wazi ya watu na viongozi wa dini mbalimbali. Wauaji wanatamba kwa jeuri na
pasipo woga wa sheria kwa sababu wana watu wao katika ofisi kuu. Tuna sadiki vyombo
vya usalama vina uwezo na nyenzo za kuwatia mbaroni wahalifu hao iwapo tu patakuwepo
na utashi wa kisiasa. Tunawasihi watu wote wenye imani; Wakatoliki, Wakristo wa
makanisa mengine yote na waumini wa kweli wa Kiislamu, sote kwa pamoja kuonyesha utashi
wetu wa kutetea na kudumisha amani tuliyopigania tokea mapambano ya uhuru. Kwa moyo
thabiti tukatae kupotoshwa na kikundi cha wachache wanaofadhiliwa na wahalifu bali
tusimame imara kujenga Tanzania inayotakiwa na wengi wetu. Madhumuni makuu ya Katiba
mpya ni kufikia muafaka wa tutakavyo kuishi kwa umoja kama taifa huru, tukikubaliana
katika tofauti zetu za asili na imani pia tukielewana vema na kustahimiliana. Jambo
hilo tunalisisitiza kwa viongozi wetu wa dini, wanaopaswa kutuongoza katika juhudi
za kujenga amani na upatanifu, kushutumu kinabii maovu na wapanga maovu ya kuvuruga
amani na upatanifu wetu. Viongozi wafafanue viini sababishi vya uvunjifu wa upatanifu
wetu ambavyo ni tofauti kubwa za kipato, uwepo wa matajiri wakubwa na masikini wa
kutupwa, ukosefu wa ajira kwa vijana na fursa za kazi za kujipatia kipato katika
kazi halali za kilimo na ufundi, wakulima wadogo kutokuwa na soko la mazao yao, n.k.
Hali hizo ndizo mazalia ambamo chuki hukua na kuwaelekeza vijana pasipo kufikiri kwenye
vurugu za kikatili na mauaji ya kinyama. Tunawaomba viongozi wetu wa dini zote
nchini kuteua siku maalumu ambayo watu wote wenye mapenzi mema watadhihirisha utashi
wao wa kulinda na kutetea amani ya nchi yetu. Jambo hilo linaweza kutekelezwa kwa
namna mbalimbali; kama vile maandamano ya amani, maandamano ya kidini, siku maalumu
ya mikutano ya wazi ya sala nchi nzima kama alivyofanya Baba Mtakatifu kule Assisi.
Umuhimu wa maadhimisho ya namna hiyo ni kusema pamoja kwa nguvu na uwazi kwamba
Watanzania wanataka amani, upatanifu na umoja katika tofauti zao asili na imani. Kwa
miaka mingi tumeishi kwa umoja na tunataka kuendelea kuishi kwa amani iliyo bora kwa
ukweli, uhuru, haki na mshikamano kwa maslahi na ustawi wa wote. Hatutaruhusu
kikundi cha wachache wetu kusababisha mageuzi ya kisiasa na kidini kwa malengo yao
na kuchukua madaraka na kutawala kidikteta. Historia ya ulimwengu na yanayojiri katika
mataifa kadhaa barani Afrika ni fundisho la kutosha na hatutaki Tanzania kuwa mhanga
wa mienendo hiyo. Fikra, maneno na ishara za amani hujenga mawazo na utamaduni
wa amani ambao kwao watu huheshimiana, huaminiana katika anga changamfu. Hilo
ndilo ombi letu kwa watu wote wenye mapenzi mema, mtuunge mkono katika jitihada zetu
za kujenga haki na amani kwa pamoja.
Dar es Salaam Februari 27, 2013 Wajumbe
wa Mkutano wa Kitaifa wa Tume za Haki na Amani za Majimbo na Wanataaluma Wakristo
Tanzania, CPT. Askofu Mkuu Paul Ruzoka Jimbo Kuu la Tabora na Mwenyekiti
wa Tume ya Haki na Amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.