2013-04-03 10:03:55

Mshuhudieni Kristo aliyeko mioyoni mwenu kwa uhalisia wa maisha!


Nimemwona Bwana! Ni maneno ya furaha yaliyokuwa yanabubujika kutoka mdomoni mwa Magdalena, yule mwanamke mdhambi, aliyethubutu kuonesha moyo wa toba kwa machozi yaliyolowanisha miguu ya Yesu, akaipangusa kwa nywele zake! Ni yule mwanamke aliyekuwa anaangaliwa kwa "jicho la kengeza" na wale waliokuwa wanajiona kuwa wenye haki, ndiye mwanamke aliyebahatika pia kupendwa na kusamehewa dhambi zake!

Anakwenda kaburini kumtafuta Yesu aliyekuwa nanga ya matumaini yake, lakini anaambulia patupu! Moyo wake unagubikwa na simanzi kuu! Machozi yanamwandaa Magdalena ili kumwona Yesu Kristo Mfufuka! Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu aliyoadhimisha katika Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae, Jumanne, tarehe 2 Aprili 2013.

Madgalena aliyekutana na kuonana na Kristo Mfufuka anashuhudia kwa furaha isiyokuwa na kifani. Mwanadamu katika hija ya maisha yake, anapitia vipindi vya furaha, majonzi na huzuni ya ndani! Je, katika mahangaiko yote haya, anauliza Baba Mtakatifu Francisko, mwamini ameweza kumwona Yesu Mfufuka akiwa kandoni mwake? Mwamini anapaswa kusikitika kutoka na dhambi zake na kufurahia pale anapopata nafasi ya kukutana na Kristo katika hija ya maisha yake.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake mafupi kwa waamini waliokuwa wamekusanyika kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae, kuomba neema ya kuweza kukutana na Yesu katika undani wa mioyo yao, ili waweze kuwa tayari kumtolea ushuhuda amini wa uwepo wake endelevu katika hija ya uhalisia wa maisha yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.