Yaliyojiri katika hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania
Ndugu Wananchi; Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai
na kunipa fursa ya kuzungumza nanyi kwa kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa kila mwisho
wa mwezi. Leo ninayo mambo matatu ninayopenda kuzungumza nanyi. Ziara ya Rais
wa China Nchini Tanzania Ndugu wananchi;
Jambo la kwanza ni ziara ya Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu
wa China aliyoifanya nchini kwetu kati ya tarehe 24 na 25 Machi, 2013. Lengo la ziara
yake ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya China na Tanzania.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wakazi wa Dar es Salaam kwa kumpokea vizuri
mgeni wetu na ujumbe wake. Wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu na
watu wake. Kwa niaba yenu, nimepokea salamu za shukrani kutoka kwa Rais Xi Jinping
akielezea kufurahishwa na mapokezi mazuri tuliyowapatia. Naomba tuendelee kuonesha
moyo wa upendo na ukarimu kwa wageni wetu wengine mashuhuri watakaotutembelea siku
za usoni. Ndugu wananchi; Nami pia, nimemshukuru sana Mheshimiwa Xi Jinping
kwa kukubali mwaliko wangu na kufanya ziara ya kihistoria na yenye mafanikio makubwa
kwa nchi yetu. Ameifanyia nchi yetu jambo la heshima kubwa na kumbukumbu isiyosahaulika.
Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuitembelea, tena siku kumi tu baada
ya kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi yake. Na, kubwa zaidi ni kutumia fursa ya ziara
yake hapa nchini kutangazia dunia Sera ya China kwa Afrika katika kipindi cha uongozi
wake. Tumefarijika sana kusikia kuwa uhusiano na Afrika bado unapewa kipaumbele
cha juu na viongozi wapya wa China. Pia, kuwa China itaendelea kukuza biashara na
uwekezaji na kuongeza misaada ya maendeleo kwa Afrika ikiwemo kutoa nafasi 18,000
za mafunzo kwa vijana wa Kiafrika. Kama mtakumbuka nchi zetu mbili zilitiliana saini
mikataka 16 ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Misaada ya maendekeo kwa maeneo
yetu ya kipaumbele nayo imejumuishwa. Ndugu Wananchi; Rais Xi Jinping alielezea
na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali na Chama cha Kikomunisti cha China ya kudumisha
na kukuza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na China. Kama mjuavyo uhusiano huo
ulianzishwa mwaka 1964 na waasisi wa nchi zetu, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong aliyekuwa Kiongozi Mkuu
wa China na Waziri Mkuu wake Chou En Lai. Rais wa China aliahidi kuwa nchi yake
itaendelea kushirikiana na Tanzania katika medani ya kimataifa na kuchangia katika
jitihada zetu za kujiletea maendeleo kwa kuongeza misaada ya maendeleo. Katika miaka
49 ya uhusiano na ushirikiano na China nchi yetu imepata misaada mingi ya maendeleo
ikiwemo Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere ambao ulizinduliwa na Rais
Xi Jinping wakati wa ziara yake. Ndugu wananchi; Kuna miradi kadhaa mikubwa
inayoendelea kutekelezwa nchini, Bara na Zanzibar, kwa msaada wa Serikali ya China.
Wakati wa ziara yake, Rais Xi Jinping iliahidi kuendelea kutusaidia miradi mingine
ya maendeleo kama tulivyoomba wakati wa mazungumzo yetu licha ya ile ambayo ilitiwa
saini siku ile. Ajali ya Kuporomoka Jengo la Ghorofa Jijini Dar
es Salaam
Ndugu Wananchi; Jambo la pili ninalotaka kuzungumzia
ni ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa katika jiji la
Dar es Salaam. Ajali hiyo iliyotokea juzi tarehe 29 Machi, 2013 imeleta msiba na
simanzi kubwa nchini. Mpaka sasa maiti za ndugu zetu 30 zimepatikana. Watu 17 waliweza
kuokolewa, wanne kati yao bado wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili. Wengine walitibiwa na kuruhusiwa. Kazi ya kufukua eneo la ajali inaendelea
na sasa inakaribia kufikia ukingoni. Ndugu Wananchi; Mimi na viongozi
wenzangu tulipata nafasi ya kwenda kuangalia eneo la ajali. Hali niliyoiona pale
imenihuzunisha sana. Lazima nikiri, hata hivyo, kwamba nimeridhishwa sana na juhudi
kubwa za uokoaji zilizokuwa zinafanywa na wanajeshi wetu wakishirikiana na taasisi,
mashirika binafsi na wananchi. Napenda kutumia nafasi kutoa shukrani maalum kwa Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Saidi Meck Sadick kwa uongozi wake madhubuti. Pia
nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Raymond Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam, Ndugu Suleiman Kova pamoja na Maafisa na askari wa JWTZ,
na wale wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika juhudi za uokoaji.
Nawapongeza pia madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali
nyinginezo kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya waliojeruhiwa. Nawapa pole wale wote
waliofiwa na wapendwa, ndugu na jamaa zao katika ajali hii. Nawaomba wawe na moyo
wa subira huku sote tukiungana nao kuwaombea marehemu wetu wapate mapumziko mema peponi.
Kwa waliojeruhiwa, tunawaombea wapone upesi. Ndugu Wananchi; Maneno
mengi yanasemwa kuhusu chanzo cha ajali ile. Alimradi kila mtu ana dhana yake. Niliagiza
vyombo na mamlaka husika wachukue hatua zipasazo kuchunguza sababu za ghorofa hilo
kuanguka na watakaothibitika kusababisha maafa hayo wachukuliwe hatua zipasazo.
Wa kushtakiwa Mahakamani washitakiwe na wa kufutiwa leseni za kufanya shughuli za
ujenzi au taaluma zao wafutiwe bila ajizi. Jambo la msingi la kusisitiza ni kuwa
mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ujenzi lazima zitimize ipasavyo wajibu wake.
Naamini kama mamlaka hizo zingetimiza ipasavyo wajibu wake ajali hii ingeepukika.
Halmashauri za miji na wilaya zina wajibu maalum kwenye ujenzi katika maeneo yao.
Watimize wajibu wao. Yaliyotokea Dar es Salaam yawe fundisho kwa wote.
Ndugu Wananchi; Ni matumaini yangu kuwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi
na Bodi ya Usajili wa Wahandisi itakamilisha mapema uchunguzi wake ili ukweli ujulikane.
Bodi ya Usajili wa Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi na Baraza la Taifa la Ujenzi
nao washirikishwe kwa ukamilifu ili ukweli upatikane na hatua stahiki zichukuliwe.
Pia naomba washauri namna bora ya kukomesha ajali za aina hiyo siku za usoni. Uhusiano
wa Wakristo na Waislamu Ndugu Wananchi; Jambo la tatu ninalopenda
kuzungumza nanyi leo ni uhusiano wa Waislamu na Wakristo nchini. Jambo hili nimeshalizungumzia
mara kadhaa siku za nyuma, lakini nalazimika kulisemea tena kutokana na hali ilivyo
sasa. Tumefikia mahali ambapo kama viongozi na waumini wa dini hizi kubwa mbili hawatakubali
kubadili muelekeo wa sasa, tunakoelekea ni kubaya. Nchi yetu nzuri tutaivuruga na
sifa yake ya miaka mingi ya Waislamu na Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa upendo,
ushirikiano na kuvumiliana itatoweka. Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia
katika orodha ya nchi zenye migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe. Ndugu
Wananchi; Nyaraka na kauli kali kali zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo
na Kiislamu zinanishawishi kuamini haya niyasemayo. Nyaraka na kauli hizo zina mambo
mawili makuu. Kwanza, kwamba kila upande unatuhumu, kushutumu na kulaumu upande mwingine
kwa kufanya vitendo viovu dhidi ya dini yake. Kauli na mihadhara ya kudhalilisha
dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu
nani achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa mifano.
Na, pili kwamba kila upande unailamu Serikali kwa kupendelea upande mwingine.
Wakristo wanalaumu kwamba mihadhara ya kudhalilisha Ukristo inaendeshwa na Serikali
haichukui hatua. Aidha, Wakristo wanateswa na viongozi wao kuuawa na Waislamu, lakini
Serikali haichukui hatua. Kwa ajili hiyo wanadai kuwa Serikali imeshindwa kulinda
uhai wa raia wake. Wanasema pia kwamba Serikali inapendelea upande wa Waislamu.
Ndugu Wananchi; Waislamu nao wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran
Tukufu, kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na Serikali
haichukui hatua yo yote ya maana. Waislamu wananyanyaswa katika nchi yao, wanakamatwa
ovyo, hawapewi fursa sawa na kwamba Serikali inawapendelea Wakristo. Wanasema nchi
inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo. Mimi binafsi wananishutumu kuwa napendelea kushiriki
zaidi kwenye shughuli za Wakristo kuliko za Waislamu kama vile harambee za kujenga
Makanisa na shule za Makanisa. Naambiwa kuwa mwepesi kushiriki maziko ya Maaskofu
kuliko Masheikh wanapofariki. Ipo Misikiti mitatu hapa Dar es Salaam wamenisomea itikafu
nife. Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema
na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi
Ndugu Suleiman Kova. Ndugu Wananchi; Napenda kuwahakikishia Watanzania
wenzangu kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza, hatupendelei upande wo wote. Hatufurahishwi
na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini
ya Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa
nyakati mbalimbali. Vyombo vya usalama vinatambua wajibu wake huo na kama haifanyiki
ni ulegevu wa mtu tu katika kutimiza wajibu wao na siyo kwamba ni sera na maelekezo
yangu au ya Serikali. Mtakumbuka kuwa mara kadhaa nimewakumbusha Wakuu wa Mikoa na
Wilaya na wakuu wa vyombo vya usalama kuacha ajizi katika kutimiza wajibu wao kwenye
suala hili. Ndugu Wananchi; Mimi binafsi sibagui, hushiriki shughuli za Waislamu
na Wakristo kila ninapoalikwa labda nikose nafasi kwa sababu nyinginezo. Nimeshafanya
shughuli nyingi za Waislamu kama vile Maulid ya Mtume Muhamad S.A.W., safari za Hija,
ujenzi wa misikiti na madrasa na mengineyo mengi. Nimeshashiriki mazishi ya Masheikh
kama nifanyavyo kwa Maaskofu na watu mbalimbali Waislamu na Wakristo. Pale ambapo
sikushiriki mazishi ya Sheikh au Askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa na shughuli
nyingine ambazo lazima nifanye mimi, au taarifa ilikuwa ya muda mfupi. Kwa upande
wa Waislamu desturi yetu ya kuzika mara mtu anapofariki huwa kikwazo kwangu kushiriki
hasa ikiwa ni nje ya Dar es Salaam kwa sababu ya taratibu za kumsafirisha Rais kutoka
mahali pamoja kwenda pengine siyo nyepesi. Wakristo hawana utaratibu huo, huwa wanaweza
kusubiri hivyo huniwia rahisi kushiriki. Ndugu Wananchi; Napenda kuwahakikishia
kuwa Serikali yetu haijashindwa kulinda usalama wa raia wake au viongozi wa dini na
nyumba za ibada. Kama ingekuwa hivyo, tungeshuhudia mauaji ya raia, viongozi wa dini
na matukio ya kuchomwa nyumba za ibada yakiwa mengi hapa nchini. Lakini hivyo sivyo.
Nawasihi sana ndugu zangu Wakristo na Waislamu kuwa tusiyachakulie matukio ya kuuawa
kwa Mchungaji Mathayo Kachila kule Buseresere, Geita, na Padri Evaristus Mushi kule
Zanzibar, au kumwagiwa tindikali Sheikh Fadhili Soroga, Naibu Mufti wa Zanizbar, kupigwa
risasi Padri Ambrose Mkenda na kuchomwa moto kwa Makanisa Zanzibar na Mbagala, Dar
es Salaam kuwa ni kielelezo na ushahidi wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake. Kila
tukio lina mazingira yake, hakuna ushahidi wa vyombo vya Serikali kuzembea. Hakuna
ushahidi wa matukio hayo kuunganika. Mpaka sasa hatujapata ushahidi wa kuwepo kikundi
cha Waislamu wanaopanga kuua viongozi wa Kikristo na kuchoma moto Makanisa hapa nchini.
Ndugu Wananchi; Kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila wa Buseresere ni matokeo
ya vurugu zilizosababishwa na mzozo kati ya Wakristo na Waislamu kuhusu kama nyama
iliyochinjwa na Wakristo Kanisani nayo iuzwe kwenye bucha iliyopo pale kijijini ambayo
kwa mazoea huuzwa nyama iliyochinjwa na Waislamu. Katika ugomvi na vurumai hizo ndipo
watu kadhaa wa pande zote walijeruhiwa na Mchungaji kupoteza maisha. Si tukio unaloweza
kulihusisha na mengineyo nchini. Ni la pale pale Buseresere na limeanzishwa na kuhusisha
Wakristo na Waislamu wa Buseresere kwa sababu zao. Hivi kama kusingekuwepo na
mzozo wa nyama ile kuuzwa katika bucha ile kuumizana kule na mauaji yale yangetokea?
Kabla ya mzozo ule Wakristo na Waislamu wa Buseresere hawakuwa na ugomvi baina yao.
Walikuwa wanaishi kidugu na kushirikiana katika shughuli zao za kujitafutia riziki
huku kila mmoja akimuabudu Mungu kwa misingi ya dini yake. Hivyo kutumia tukio hilo
kutoa wito kwa Wakristo wote kuwa kuuawa kwa Mchungaji Kachila ni sawa na kuuawa kwa
Wakristo wote nchini kulikofanywa na Waislamu ni kulikuza tatizo isivyostahili. Busara
ituongoze kutafuta njia ya kuwapatanisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere wazungumze,
waelewane na waendelee kuishi pamoja kama ilivyokuwa awali. Hata mzozo wa kuchinja
wanaweza kuumaliza. Mbona bucha za kitimoto zipo na watu hawajapigana. Kutumia mzozo
wa Buseresere kueneza chuki kati ya Wakristo na Waislamu nchi nzima si sawa. Hatuwatendei
haki Watanzania.
Ndugu Wananchi; Kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi
wa Zanzibar ni tukio linalojitegemea halina uhusiano kabisa na lile la Buseresere,
Geita. Hapakuwa na mzozo kuhusu nani achinje. Bado uchunguzi wake unaendelea na
tumehusisha vyombo vya upelelezi vya nje vishirikiane na vyetu kufanya uchunguzi.
Tumefanya hivyo kwa sababu ya ugumu uliopatikana katika uchunguzi wa matukio ya kabla
yake. Yaani ile la kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa Padri Ambrose Mkenda na kumwagiwa
tindikali kwa Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili Soroga. Bado hakuna mafanikio
ya kutia moyo. Na bado tunajiuliza kama matukio hayo matatu yanahusiana. Je, Makanisa
kuchomwa moto kule Zanzibar nako kuna uhusiano wowote na matukio yale matatu? Uchunguzi
unaoendelea unaweza kufumbua fumbo hilo. Kuna watu wanadhani yanahusiana na
kwa sababu nzuri. Lakini inabaki kuwa ni dhana ya kibinadamu mpaka ukweli halisi
utakapobainika. Bado kazi ya uchunguzi inaendelea kufanywa na vyombo vya usalama
vya nchi yetu wakishirikiana na wenzao wa nje. Katika mazingira hayo, ni mapema mno
kumnyooshea kidole mtu ye yote na kuilaumu Serikali ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar. Serikali siyo mshirika katika mauaji hayo, na haina sababu ya kufanya
hivyo. Ndiyo maana tunahangaika usiku na mchana kupata jawabu. Ndugu Wananchi;
Hali kadhalika tukio la Makanisa ya Mbagala, Dar Es Salaam kuvamiwa, kubomolewa, mali
kuibiwa na kuchomwa moto tarehe 12 Oktoba, 2012 nalo lina mazingira yake maalum.
Chanzo chake ni mzozo uliotokana na tukio la kusikitisha la kijana mmoja Mkristo kukojolea
Kitabu Kitakatifu cha Waislamu, yaani Quran Tukufu. Pamoja na maelezo kuwa walikuwa
na ubishi wa kitoto na kijana mwenzake, lakini kitendo hicho kiliwakasirisha Waislamu.
Kijana huyo alifikishwa kituo cha Polisi. Baadhi ya Waislamu wenye msimamo mkali
walifika kituoni hapo wakidai wapewe huyo kijana wamuadhibu wao. Jeshi la Polisi
lilikataa. Kukatokea mzozo kati ya waumini hao na Polisi na baada ya kushindwa walichokitaka
baadhi yao walipotoka pale, wakaenda kufanya uhalifu wa kuvunja, kuiba na kuchoma
moto Makanisa. Ndugu Wananchi; Baada ya tukio la Mbagala hapajakuwepo na tukio
la kuchomwa Kanisa mahali popote kwa upande wa Bara. Aidha, hapajawahi kuwepo tishio
lililothibitika la watu kutaka kuchoma Kanisa popote. Lakini maneno ya vitisho vya
kuchoma Makanisa yako mengi hasa kupitia mitandao ya simu za mkononi. Kila ujumbe
wa namna hiyo ulipofikishwa kwenye vyombo vya usalama uchunguzi umefanywa na hata
hatua za tahadhari kuchukuliwa lakini hakuna hata taarifa moja iliyothibitika kuwa
na chembe ya ukweli. Hata dalili hazijakuwepo. Tulichojifunza ni kuwa ujumbe
na vitisho vya aina mbalimbali hupelekwa kote, kwa Wakristo na Waislamu. Upo unaowalenga
Wakristo ukiwaambia wenzao Waislamu wanapanga kuwadhuru. Na upo wanaopelekewa Waislamu
wakiambiwa Wakristo wanao mipango mibaya dhidi yao. Watanzania wenzangu nawaomba
mtanabahi na mjue kuwa wapo watu wanacheza mchezo mchafu wa kuwagonganisha na kutaka
kuwagombanisha Wakristo na Waislamu kwa sababu wanazozijua wao na kwa faida yao.
Wanapandikiza chuki kwa lengo la kutaka Wakristo na Waislamu wagombane. Wanapandikiza
chuki baina ya Serikali na waumini wa dini zetu kuu mbili ili ionekane Serikali imewatelekeza
raia wake. Ni mchezo mbaya, tusikubali kucheza ngoma tusiyoijua. Hivi ndugu zangu
mmekaa chini na kujiuliza kumetokea nini kipya hata leo kuwa na mhemko kama huu kati
ya Wakristo na Waislamu na kutishia kuleta vita baina nchini kote?
Ndugu Wananchi;
Serikali haijapuuzia kila palipotokea matukio ya uhalifu. Watu 76 wanaotuhumiwa kuharibu
na kuchoma moto Makanisa kule Mbagala na kufanya fujo kituo cha Polisi wamekamatwa
na kesi zao zinaendelea Mahakamani. Kwa upande wa tukio la Buseresere lililosababisha
kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila, watu 17, wakiwemo waumini wa dini ya Kikristo
na Kiislamu walikamatwa na kesi zao zinaendelea. Wapo walioshitakiwa kwa mauaji na
wapo walioshitakiwa kwa kufanya vurugu. Jeshi la Polisi bado linawatafuta watu wengine
waliohusika na uhalifu huo ili na wao wakamatwe. Kwa upande wa Zanzibar, watu 10 wanaotuhumiwa
kuchoma Makanisa wamekamatwa na kesi zao zinaendelea. Bado hajakamatwa mtu kwa tukio
la mwisho la kuchoma Kanisa baada ya kuuawa Padri Evaristus Mushi. Uchunguzi unaendelea. Ndugu
Wananchi; Kwa upande wa kujeruhiwa kwa Padre Mkenda, bado uchunguzi haujakamilika
pamoja na kuwapo taarifa kadhaa zinazoendelea kufanyiwa kazi. Kuhusu uchunguzi wa
mauaji ya Padre Mushi, baada ya jitihada kubwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kushirikisha
nchi zilizobobea katika uchunguzi wa makosa ya aina hii, hatua ya kutia moyo imefikiwa.
Mtu mmoja amekamatwa na wengine wanaendelea kutafutwa. Ndugu Wananchi; Kwa
upande wa kanda na vituo vya redio nako pia Serikali imechukua hatua. Watu kadhaa
wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kurekodi
na kusambaza kanda zinazochochea chuki na vurugu za kidini. Wapo Waislamu na Wakristo.
Wapo watu wengine ambao wanaendelea kutafutwa. Zipo taarifa kuwa baadhi yao wamekimbilia
nchi za nje. Jeshi la Polisi limeomba msaada wa Polisi wa Kimataifa, yaani Interpol,
kusaidia kuwatafuta na kuwarejesha nchini. Vituo viwili vya radio yaani Kwa Neema
FM cha Sengereme na Radio Imani cha Morogoro vimefungiwa kwa muda wa miezi sita.
Baada ya muda huo kupita, Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano itaamua ipasavyo. Ndugu
Wananchi; Nimeyaeleza haya kwa kirefu kuwahakikishia kuwa Serikali inajali
usalama wa raia wake wa mali zao na amani na utulivu wa nchi yetu. Kamwe hatujashindwa
kulinda raia wa nchi wa yetu na yapo mambo mengi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika
kuhakikisha kuwa Watanzania wa dini zote, makabila yote, rangi zote na mahali po pote
walipo wako salama. Tunataka kuona watu wanaendelea kuishi kwa amani, upendo, ushirikiano
na mshikamano kama tulivyokuwa tunaishi siku zote. Tunapenda kuona Watanzania wanaepuka
mambo yanayowabagua na kusisitiza yale yanayowaunganisha. Tujiepushe kuyapa kipaumbele
yale yanayotugawa. Ndugu Wananchi; Athari za mzozo kuhusu kuchinja kule
Geita iwe fundisho kwetu sote. Tuazimie sote kuwa yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.
Hebu tufikirie maisha yetu Watanzania yatakuwaje kwenye shughuli za kijamii kama vile
sherehe, harusi, ngoma na misiba iwapo tutaanza kuwa na chakula tofauti kwa Waislamu
na Wakristo. Fikiria itakuwaje kwenye hospitali, shule na vyuo pawe na majiko mawili
au labda hata mabwalo mawili ya chakula kwa Waislamu na Wakristo. Jeshini nako kuwe
na majiko na mabwalo ya Waislamu na Wakristo. Hali iwe hivyo hivyo kwenye migahawa
na maeneo mengine yenye huduma ya chakula. Ndugu zangu, tunataka kuipeleka wapi
nchi yetu? Tunataka kujenga nchi ya namna gani? Mimi naamini tukifanya hivyo huo utakuwa
ndiyo mwanzo wa kubaguana kwa kila kitu na kila jambo na kuligawa taifa kwa namna
ambayo hatutakuwa wamoja tena. Huko tunakoelekea siko, ni kubaya. Tubadilike, na
wakati ni huu. Viongozi wa dini waongoze njia wawaepushe waumini wao na taifa letu
na janga hili. Ndugu Wananchi; Bado narudia kusisitiza umuhimu wa
viongozi wa dini zetu kubwa mbili kukutana na kuizungumzia hali hii na kuipatia ufumbuzi.
Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote wenye majawabu ya matatizo haya. Ni masuala yanayohusu
imani za dini na yanafanywa na viongozi wa dini na wafuasi wao kwa jina la dini zao.
Serikali ina wajibu wa kulinda amani. Kazi yetu itakuwa rahisi kama waumini hawatafanya
vitendo vitakavyosababisha uvunjifu wa amani. Wa kuongoza waumini lipi jema na lipi
baya ni viongozi wa dini. Ndugu Wananchi; Nimeshakutana na viongozi kadhaa
wa madhehebu na taasisi za dini za Kikristo na Kiislamu kuzungumza nao kuhusu jambo
hilo. Nimepata faraja kuona kuwa wote wanasikitishwa na mambo yanayotokea hivi sasa
na wameona busara ya viongozi wa dini kuzungumza ili kuondoa tofauti zilizojitokeza.
Wanakiri kuwa hali ilivyo sasa siyo ya kawaida kwa Tanzania na Watanzania. Kuna upepo
mbaya wa shetani unapita ambao viongozi wa dini wana wajibu wa kuhakikisha kuwa hali
ya hewa inasafishwa na kurejesha nchi yetu na watu wake katika maisha tuliyoyazoea.
Maisha ambayo waumini wa dini tofauti wanaishi pamoja kwa udugu, upendo, ushirikiano
na mshikamano kwa misingi ya ubinadamu wao na Utanzania wao. Waziri Mkuu, Mheshimiwa
Mizengo Pinda, ameshaeleza dhamira ya Serikali ya kuitisha mkutano wa viongozi wa
dini mapema mwezi ujao. Ni matumaini yangu kuwa wote watashiriki wenyewe bila ya
kutuma wawakilishi. Lazima tupate jawabu kwa maslahi ya taifa letu na watu wake. Ndugu
Wananchi; Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kutumia nafasi hii kuwaomba
na kuwasihi waandishi wa habari wasaidie kuliepusha taifa letu kuingia katika vita
vya kidini. Waache kushabikia taarifa zinazochochea na kujenga uhasama baina ya waumini
wa dini zetu. Nawaomba wapime athari za taarifa zao kabla ya kuziandika au kuzitangaza.
Wawe makini na maneno wanayotumia. Katika hali tuliyonayo sasa lazima sote tuazimie
kuondoa tofauti za kidini na kujenga umoja miongoni mwa Watanzania wa dini zote.
Wasipofanya hivyo, wataliingiza taifa katika mgogoro mkubwa ambao hauna msingi kama
ilivyotokea katika nchi jirani. Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari kutambua kuwa
wanao wajibu wa kuhakikisha vyombo vyao havitumiki kuleta mifarakano kwa kuchochea
uhasama baina ya Wakristo na Waislamu. Hitimisho Ndugu Wananchi;
Naomba kumaliza kuwa kusisitiza kuwa wananchi wote kudumisha umoja na mshikamano wetu.
Tuishi kwa upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini zetu,
kabila, rangi au mahali atokako mtu. Hizo ndizo tunu za taifa letu la Tanzania ambazo
hatuna budi kuzienzi, kuzilinda na kuzidumisha. Narudia kuwahakikishia kuwa Serikali
haipendelei dini yo yote na wala haina mpango wa kushiriki kuangamiza dini yo yote
au waumini wao. Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama itaendelea kuhakikisha
ulinzi na usalama wa raia wake na mali zao kama inavyofanya siku zote. Kama kuna
mtu anaona kuwa maisha yake au mali zake zipo hatarini, aende kutoa taarifa Polisi.
Hatua zipasazo zitachukuliwa. Ndugu Wananchi; Mwisho nawatakia sikukuu njema
ya Pasaka. Tusherehekee kwa amani na utulivu. Tusherehekee pamoja.
Mungu
Ibariki Afrika! Mungu Ibariki Tanzania! Asanteni kwa Kunisikiliza.