Vijana wapewa changamoto ya kujiamini katika kushiriki mchakato wa maisha bora zaidi;
waachane na matumizi haramu ya dawa za kulevya!
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon, tarehe Mosi Aprili 2013, ametembelea
Jumuiya ya Mtakatifu Patrignano, iliyoko Rimini, Italia inayojihusisha na utoaji wa
tiba kwa vijana walioathirika kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya na kuwaomba
wahudumu katika Jumuiya hii kuwa na moyo wa huruma na uchungu wanapowahudumia vijana
hao wanaofanya hija ya kurekebisha maisha yao, ili kuwa watu wema zaidi.
Jumuiya
hii inatoa huduma kwa vijana 1,300 kutoka katika mataifa 28 ambao wamejikuta wakitumbukia
katika matumizi haramu ya dawa za kulevya. Katibu mkuu alichukua fursa hii kufungua
kinywa pamoja nao na kukumbusha kwamba, hakuna binadamu ambaye ni mkamilifu, kila
mtu anaweza kukosea, lakini jambo la msingi kwa vijana hawa kwa sasa ni kuibua karama
na vipaji walivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu ili kuvikuza na hatimaye, kuvitumia kwa
ajili ya mafao yao na Jamii inayowazunguka. Muda walionao hapo kituoni, iwe ni fursa
ya kukomaa na hatimaye, kuachana kabisa na matumizi haramu ya dawa za kulevya kwani
zina madhara makubwa kwa binadamu.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema,
takwimu za idadi ya watu duniani zinaonesha kwamba, nusu ya vijana wote duniani ni
wale walio na umri chini ya miaka ishirini na mitano, wanaosoma na wengine wanafanya
kazi mbali mbali ili kuwa na leo na kesho iliyo bora zaidi. Amewataka vijana kuwa
na ujasiri na imani kwa ajili ya maisha yao kwa sasa na kwa siku za usoni na kwamba,
Jumuiya ya Kimataifa iko bega kwa bega pamoja nao!