2013-04-02 08:29:00

Papa atembelea Kaburi la Mtakatifu Petro, chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe Mosi Aprili 2013 jioni, ametembelea kwenye Makaburi yaliyoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Kumbu kumbu zinaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni Papa wa kwanza kutembelea makaburi haya ambayo yamekuwa ni kivutio kikuu kwa wataalam wa mambo ya kale na watalii kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwani huko ndiko kunakosadikiwa kwamba, kuna Kaburi la Mtakatifu Petro, mwamba wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko katika matembezi yake kwa takribani dakika 45 hatimaye, alifika kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro. Baadaye pembeni kidogo kwenye Kikanisa cha Clemetina hapo alisali kwa kitambo kidogo. Itakumbukwa kwamba, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro limejengwa kwenye kilima ambacho Wakristo wa Kanisa la mwanzo, walikuwa wanakusanyika ili kusali kwa kificho wakati wa madhulumu ya Wakristo kwenye utawala wa Kirumi.

Katika matembezi haya, Baba Mtakatifu Francisko alifuatana na Kardinali Angelo Comastri, mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro pamoja na baadhi ya viongozi waandamizi kutoka Vatican. Kwa pamoja walipita kwenye njia nyembamba zilizokuwa zinatumiwa na Wakristo wakati huo.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha matembezi yake ya kiroho kwa kusali kwenye Makaburi ya watangulizi wake yaliyoko kwenye Pango la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Hawa ni Papa Benedikto wa kumi na tano, Pio wa kumi na mbili, Paulo wa sita na Yohane Paulo wa kwanza. Baada ya kutoka ndani ya Makaburi hayo, Baba Mtakatifu Francisko alisalimiana na baadhi ya wafanyakazi waliokuwapo katika eneo hili na baadaye alirejea kwenye makazi yake ya muda huku akifanya mazoezi ya kutembea kwa miguu!

Kunako mwaka 1939 Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili aliagiza wataalam wa mambo ya kale kufanya uchunguzi wa kisayansi kuhusu Mapokeo yaliyokuwa yanaonesha kwamba, chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kulikuwa na kaburi la Mtakatifu Petro; mahali ambapo Altare kuu ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro imejengwa juu yake. Uchunguzi wa kisayansi uliofanywa ndani ya Kanisa hili, uligundua kwamba, kulikuwepo pia Makaburi 22 yaliyokuwa yamesambaa katika urefu wa mita 70, chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro.

Viongozi wa Kanisa kunako mwaka 1998 wakaamua kufanya ukarabati mkubwa ili kuhifadhi utajiri huu mkubwa katika ushuhuda wa maisha ya Wakristo wa Kanisa la Mwanzo, kazi ambayo ilihitimishwa na hatimaye, kufunguliwa Mwezi Mei, 2008.

Baba Mtakatifu Francisko kwa matembezi haya wakati huu wa Kipindi cha Pasaka ni changamoto ya kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji Mpya katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, kwa kuendeleza ari na moyo wa Wakristo wa kwanza waliojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.

Mtakatifu Petro mwamba wa imani, alisulubiwa miguu juu na kichwa chini, mahali ambapo kunasadikiwa kwamba, kumejengwa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican







All the contents on this site are copyrighted ©.