Watu waliofariki dunia kwa kuporomokewa Jengo Dar es Salaam wanazidi kuongezeka
Taarifa ya Serikali ya Tanzania iliyonukuliwa na Shirika la Habari la AP inabainisha
kwamba, hadi kufikia Jumatatu asubuhi, tarehe Mosi, Aprili 2013, maiti 32 zilikuwa
zimekwishatolewa kwenye Jengo lililoporomoka wiki iliyopita. Matumaini ya kuwapata
watu waliofukiwa na kifusi wakiwa hai yanazidi kufifia. Inasikitisha kuona kwamba,
Jengo hili lenye ghorofa 16 lililokuwa linakaribia kumalizika limekuwa ni chanzo cha
vifo vya watu wasiokuwa na hatia, wakiwamo watoto waliokuwa wanacheza katika eneo
hili.
Mashahidi wanasema, bado kuna watu wengi ambao wamefukiwa na kifusi
katika jengo hili. Katika miaka ya hivi karibuni kuporomoka kwa majengo katika baadhi
ya nchi za Afrika Mashariki linaonekana kuwa ni jambo la kawaida kutokana na ukweli
kwamba, baadhi ya wamiliki na makandarasi wanapindisha sheria na kutaka kubana matumizi,
matokeo yake ni maafa kwa watu wasiokuwa na hatia!