2013-04-01 08:29:05

Ujumbe wa Siku kuu ya Pasaka kutoka kwa Viongozi wakuu wa Makanisa Nchi Takatifu


Viongozi wakuu wa Makanisa ya Kikristo walioko katika Nchi Takatifu, katika ujumbe wao wa Kiekumene katika Kipindi cha Pasaka, wanawaalika waamini na mahujaji na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia kutembelea Makanisa yao, ili kufanya hija ya imani huku wakifuata nyayo za Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. RealAudioMP3
Mji wa Yerusalemu ni kielelezo cha imani ya Kristo Mfufuka, aliyeshuhudiwa na Mitume wake, walipogundua kwamba, kwa hakika Kaburi lilikuwa wazi na Yesu alikuwa amefufuka kutoka katika wafu, kadiri ya Maandiko Matakatifu. Hii ni changamoto ya kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya wananchi wanaoishi kwenye Nchi takatifu.
Viongozi wakuu wa Makanisa, wanawaalika viongozi wa Serikali na Jumuiya za Kimataifa, kusimama kidete kulinda na kutetea haki, amani na upatanisho miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Kwa namna ya pekee, Viongozi hawa wanasali kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki, lakini zaidi katika nchi ya Syria, Lebanon na Palestina, Israeli na Misri; nchi ambazo zinaendelea kushuhudia kinzani na migogoro ya kivita.
Viongozi hawa wanasali kwa ajili ya wale wote wanaodhulumiwa haki zao msingi, wafungwa, watu wanaoishi katika hali ya wasi wasi kutokana na mashaka ya usalama wa mali na maisha yao; wanawakumbuka wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi wanaoendelea kuteseka huko Mashariki ya Kati.
Kwa namna ya pekee, wanasikitika kwa ajili ya Mahujaji ambao hawataweza kufanya hija ya maisha yao ya kiroho kwenye Nchi Takatifu kutokana na sababu mbali mbali na wanawaomba waendelee kuonesha mshikamano wao kwa njia ya sala, wakizidi kuwaombea Wakristo ili waweze kubaki katika maeneo yao kwani idadi ya wakristo inaendelea kupungua siku hadi siku kutokana na kinzani pamoja na madhulumu ya kidini.
Viongozi wa Makanisa wanaendelea kuhimiza umuhimu wa waamini na watu wenye mapenzi mema kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu. Washinde kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi au kujihusisha na ghasia kwa namna yoyote ile! Watambue kwamba, Yesu alikuwa ni Mfalme wa Amani.
Kwa mara ya kwanza Wakristo wanaoishi kwenye Nchi Takatifu kutokana na majadiliano na uamuzi wa kiekumene uliofanyika kunako tarehe 15 Oktoba 2012, kwa pamoja wataadhimisha Siku kuu ya Pasaka, hapo tarehe 5 Mei 2013, sanjari na Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka ya Wayahudi, kama sehemu ya majaribio ya Kiekumene.
Miji ya Bethlehemu na Yerusalemu itaendelea kufuata Kalenda ya Gregoriani, wakati ambapo sehemu nyingine watafuata Kalenda ya Juliani. Muungano wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kwa pamoja, unalenga kutoa ushuhuda wa matunda ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Makanisa mbali mbali ya Kikristo katika Nchi Takatifu pamoja na waamini wa dini ya Kiyahudi.








All the contents on this site are copyrighted ©.