2013-04-01 14:20:56

Neema ya Sakramenti ya Ubatizo na Umoja katika Ekaristi Takatifu inawawezesha waamini kuwa kweli ni vyombo vya huruma ya Mungu


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu ya Pasaka, wakati waamini wengi wakiwa bado wanasherehekea Siku kuu ya Pasaka, kwa mara nyingine tena aliungana na waamini waliofurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ili kusali pamoja Sala ya Malkia wa Mbingu inayotumika katika Kipindi cha Pasaka. Katika tafakari yake Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Pasaka ni kiini cha Imani ya Kanisa na kwamba, nguvu ya Kristo Mfufuka iwafikie watu wote wanaoteseka; wale ambao wanahitaji kuimarishwa katika imani na matumaini.

Baba Mtakatifu anasema, Kristo ameshinda uovu kwa daima, ni changamoto na mwaliko kwa waamini wa kila nyakati kuupokea ujumbe na kuumwilisha katika uhalisia wa maisha katika historia na Jamii inayowazunguka. Anawaalika kwa namna ya pekee Wakristo waliobatizwa katika: Kesha na Siku kuu ya Pasaka kwa Mwaka huu kushuhudia imani waliyoipokea kutokana na Sakramenti za Kanisa.

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, watu wanafanyika kuwa ni watoto wateule wa Mungu; Ekaristi takatifu inawaunganisha na Kristo kwa njia ya uhalisia wa maisha yake: kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo yao. Neema inayobubujika kutoka katika Sakramenti za Pasaka ina nguvu ya kumkirimia mwamini mabadiliko ya ndani kama mtu binafsi, familia na katika mahusiano ya kijamii.

Yote haya yanatendeka kwa njia ya moyo wa mwanadamu, ambao uko tayari kupokea neema kutoka kwa Kristo Mfufuka ili kubadilika na kuwa mtu mwema zaidi kwa kutambua kwamba, ubaya unaweza kumtenda mtu mwenyewe pamoja na jirani zake. Ni mwaliko wa kuhakikisha kuwa nguvu na ushindi wa Kristo mfufuka unabaki na kutenda kazi ndani ya wafuasi wake na hivyo kuenea na kuwasaidia watu wengine zaidi. Bila neema ya Mungu, hakuna jambo linalowezekana.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, kwa njia ya neema ya Sakramenti ya Ubatizo na Umoja katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, waamini wanaweza kuwa kweli ni vyombo vya huruma ya Mungu. Waamini wanakabiliwa na utume ambao unawasukuma kuhakikisha kwamba, wanamwilisha Sakramenti za Kanisa katika uhalisia wa maisha yao. Waamini wafurahie fursa ya kuwa ni vyombo vya neema ya Kristo, kama matawi yanayosimikwa katika Kristo ambaye kimsingi ndiye shina lenyewe, linalorutubisha na Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kusali kwa njia ya jina la Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, ili kwa njia ya maombezi ya Bikira Maria Fumbo la Pasaka liweze kutenda kazi ndani yao, kwa nyakati hizi, ili chuki na uhasama vitoe nafasi kwa upendo; uongo utoweke na ukweli uweze kutawala; kisasi kiache nafasi kwa fadhila ya msamaha; huzuni igeuke kuwa furaha.

mara baada ya kutafakari na kusali kwa pamoja Sala ya Malkia wa Mbingu, kwa mara nyingine tena Baba Mtakatifu Francisko, amewasalim na kuwatakia kila la kheri na baraka wakati huu Kanisa linapotangaza kwa nguvu Kristo amefufuka. Pasaka Njema.







All the contents on this site are copyrighted ©.