2013-04-01 09:49:12

Haki, amani, upendo, mshikamano na uvumilivu ni kati ya changamoto zilizotolewa na viongozi wa Makanisa katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka


Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka nchini Tanzania imekuwa ni fursa nyingine kwa viongozi mbali mbali wa Kikristo kukazia kwa namna ya pekee kabisa, mambo msingi yanayowaunganisha watanzania yaani: amani, upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Ni wajibu wao kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wajitahidi kutafuta mafao na ustawi wa watanzania wote na kamwe tofauti zao za kidini, kikabila au mahali anapotoka mtu kisiwe ni chanzo cha choko choko na vurugu nchini humo.

Katika Maadhimisho ya Pasaka Kitaifa nchini Tanzania, Ibada iliyoongozwa na Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, amewataka watanzania kujenga na kuimarisha utamaduni wa upendo na imani yao kwa Mwenyezi Mungu na kamwe wasiache mchakato wa kuandika katiba Mpya ya Tanzania ukatekwa na watu wachache kwa mafao binafsi, kwani watawatumbukiza watanzania mahali pabaya.

Askofu Nyaisonga anasema, kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, utawala wa sheria na demokrasia; maadili na utu wema. Mahakama itekeleze wajibu wake kwa kuzingatia maadili na weledi. Maliasili itumike kwa ajili ya mafao na maendeleo ya watanzania wote. Wananchi wawe makini kusikiliza na kupima hoja zinazotolewa dhidi ya Muungano wa Tanzania.

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, kwa upande wake, amekazia umuhimu wa wananchi kuheshimiana na kuthaminiana kama njia ya kukata mzizi wa fitina na chokochoko za kidini ambazo kwa miaka ya hivi karibuni zimelitikisa Taifa la Tanzania. Waamini wajenge utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia ya kutatua migogoro na kinzani zinazoibuliwa katika masuala ya kidini.

Ni wakati muafaka kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatolea ushuhuda wa imani yao kwa njia ya matendo, wakikumbuka kwamba, Yesu mwenyewe aliteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Yesu Kristo ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa mwanadamu, changamoto kwa waamini kuendelea kutenda mema, hata kama wanalipwa na mabaya!

Kardinali Pengo katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka, amezindua Parokia Mpya ya Yohane wa Mungu, Vituka, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Askofu Agostino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar anaendelea kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kuimarisha utamaduni wa: haki, amani, upendo na upatanisho na kwamba, tabia ya chuki, uhasama na moyo wa kutaka kulipizana kisasi usipewe mwanya katika maisha na vipaumbele vyao. Wananchi wanapaswa kuvumiliana hasa katika tofauti zao za kidini.

Katika Ibada za Jumapili ya Pasaka, viongozi mbali mbali wa Kikristo wametumia nafasi hii kuendelea kuhimiza amani kwa kuitaka pia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuimarisha uhuru wa kuabudu mintarafu Katiba ya Nchi. Wananchi wanatambua kwamba, ulinzi na usalama ni jukumu lao wote, lakini Serikali inawajibu wa kuhakikisha kwamba, wananchi na mali zao wanakua salama. Vitisho vya mashambulizi dhidi ya waamini wa dini moja vinapaswa kuchukuliwa kwa uzito unaostahili.







All the contents on this site are copyrighted ©.