Hali ni shwari, baada ya watu wawili kupoteza maisha Kisumu!
Watu wawili wamepoteza maisha mjini Kisumu, baada ya Mahakamu kuu ya Kenya, Jumamosi
jioni tarehe 30 Machi 2013 kutangaza kwamba, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, alikuwa
amechaguliwa kwa kura halali. Vifo hivi vimetokea mjini Kisumu inayosadikiwa kuwa
ni ngome kuu la Raila Odinga aliyekuwa amekata rufaa Mahakama kuu kupinga uchaguzi
mkuu wa Rais.
Vijana na washabiki wa Raila Odinga hawakufurahia na uamuzi
wa Mahakama kuu na hivyo wakajikuta wanakabiliana uso kwa uso na vikosi vya kutuliza
ghasia nchini Kenya. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, limeendelea kuwataka wananchi
wa Kenya kulinda na kudumisha amani na utulivu kama kikolezo cha maendeleo endelevu.
Machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza kunako mwaka 2007 liwe ni onyo kali kwa wanasiasa
na wananchi wanaotaka kuitumbukiza tena Kenya katika machafuko ya kisiasa.
Taarifa
ya Jeshi la Polisi siku ya Jumapili asubuhi ilionesha kwamba, amani na utulivu vimerudi
tena kwenye maeneo ambayo yalionekana kuwa na cheche za vurugu za kisiasa.