2013-03-30 07:03:59

Tunahesabiwa haki kwa njia ya imani katika Damu Azizi ya Yesu Kristo!


Padre Raniero Cantalamessa, katika mahubiri yake kwa Maadhimisho ya Ijumaa Kuu, tarehe 29 Machi 2013, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Kanisa linapofanya kumbu kumbu ya Mateso na Kifo cha Kristo, Ibada ambayo imehudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko, amekazia kwa namna ya pekee kwamba, waamini wanahesabiwa haki kwa njia ya imani katika Damu Azizi ya Yesu Kristo.

Mada hii inakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ambayo inaokoa na kuushinda ulimwengu, pale Mwenyezi Mungu anaponyoosha mkono wa neema na baraka kwa mwanadamu, kiasi cha kuanzisha agano jipya na la milele.

Hapa waamini wanachangamotishwa kufungua malango ya mioyo yao ili kumwamini Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili hatimaye, kumhesabia haki mwanadamu. Yesu Kristo ni chemchemi ya maisha mapya. Ibada hii pia ni mwanzo mpya wa utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, changamoto na mwaliko wa kumtambua na kuthamini uwepo wa Kristo katika hija ya maisha ya kila mwamini.

Waamini watambue dhambi na mapungufu yao, wawe tayari kuyakiri kama alivyofanya yule mtoza ushuru aliyerudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki, akiwa anatembea katika utu mpya. wakishahesabiwa haki itokayo katika imani, waamini wawe na amani kwa Mungu, kwani kwa njia ya Yesu Kristo wanaweza kufurahia na kutumainia utukufu wa Mungu, wakijua kwamba, dhiki kazi yake ni kuleta saburi na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yao kwa njia ya Roho Mtakatifu waliyempokea.

Kwa njia ya kifo na ufufuko wa Yesu Kristo anasema Padre Cantalamessa, dunia imefikia hitimisho lake, kwani Yesu Kristo amepaa kurudi kwa Baba yake wa mbinguni na anakaa kuumeni kwake. Hapa ni mwanzo wa mbingu na dunia mpya, licha ya uwepo wa taabu, magumu na hata kifo, lakini haya ni mambo ambayo Yesu ameyashinda na ni Bwana wa yote. Yesu ameshinda kifo na kifo hakina nguvu tena. Imani ya Kikristo liwe ni jibu makini katika changamoto na kinzani mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Msalaba wa Kristo uwe ni kiungo makini miongoni mwa waamini katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, kwa kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu kwamba, Yesu amewakomboa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Kwa njia ya mateso na kifo chake, Yesu anawatuma wafuasi wake kuwatangazia wote Habari Njema ya Wokovu, ili waweze kuyainua macho yao wapate kumtaza yule waliyemchoma ubavuni kwa mkuki!

Ni changamoto kwa waamini kutangaza habari ya faraja na wokovu unaobubujika kutoka kwa Kristo. Uinjilishaji ni zawadi ya Msalaba wa Kristo, unaodhihirisha Moyo wake Mtakatifu uliotobolewa humo ikatoka damu na maji, kielelezo cha upendo wa hali ya juu kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huu ni mwaliko wa kutangazia watu huruma na upendo wa Mungu, wakitambua kwamba, Uinjilishaji kwa hakika ni zawadi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, inayopania kujenga na kuimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Msalaba wa Kristo umevunjilia mbali utengano uliokuwapo kati ya waamini wa Makanisa mbali mbali, urasimu, ibada, sheria na kanuni zilizopitwa na wakati. Hii ni changamoto kwa Mama Kanisa kutoka na kuwaendea wale walioko pembezoni mwa jamii, wanaokabiliwa na uwepo wa dhambi, magumu, ukosefu wa haki msingi za binadamu, ujinga, umaskini, maradhi, kinzani za kidini na madhulumu mbali mbali.

Hiki ni kipindi cha kusoma alama za nyakati, tayari kuibua mikakati ya kichungaji, inayopania kujenga na kuimarisha Kanisa la Kristo, kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu anawasaidia kutekeleza wajibu huu msingi kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa. Kuna matumaini makubwa kwa Kanisa kuanza kipindi kipya cha maisha na utume wake; kipindi ambacho kina sheheni matumaini na watu wako tayari kuyapokea matumaini haya anasema Padre Raniero Cantalamessa, hata kwa gharama ya maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.