2013-03-30 09:09:15

Simameni kidete kulinda na kutetea imani, haki, uadilifu pamoja na kutekeleza utashi wa Mungu katika maisha yenu!


Wakristo wamekumbushwa kuishi maisha yanayoonesha shukrani na utii kwa Mwenyezi Mungu ili maisha, Kifo na ufufuko wa Yesu Kristo viweze kuonekana mioyoni mwao. Wito huo umetolewa na Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo la Iringa katika mahubiri yake kwa waamini wa Kanisa la Mtakatifu Yosefu Parokia ya Ipogolo Jimboni Iringa, alipokuwa akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Alhamisi kuu, tarehe 28 Machi 2013.
Askofu Ngalalekumtwa ambae pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amesema, ujio wa Yesu Kristo hapa Duniani ni mpango na huruma ya Mungu wa kumkomboa mwanadamu ili atoke katika utumwa wa dhambi na mauti kwa kumwongokea Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo. Amesema kitendo cha kukombolewa kwa Mwanadamu kwa njia ya mateso kifo na ufufuko wa Yesu Kristo inaonyesha ukuu wa wema, upendo, na huruma ya Mwenyezi Mungu kwa watu wote wenye taabu na shida mbalimbali katika ulimwengu mamboleo.
Askofu Ngalalekumtwa amesema kuwa Yesu Kristo katika maisha yake hapa Duniani alijishusha hadi kiasi cha kuwa mtumwa kwa Wanadamu ikiwa nipamoja na kuutoa uhai wake juu ya msalaba na kufa kifo cha aibu kwaajili ya Watu wote ili kuwafundisha kuwa na upendo na huruma kwa wengine.
Katika kipindi hiki cha kutafakari huruma ya Mungu ni vizuri Wakristo wakatumia fursa hii kumrudia Mwenyezi Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani huku wakikumbatia neema zake ili waweze kufurahia matunda ya ukarimu, upendo na utakatifu wake.
Askofu Ngalalekumtwa amewataka Wakristo kwa namna ya pekee katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kuwa na msimamo katika kulinda na kutetea Imani, Haki, na Uadilifu na kutenda yale yanayompendeza Mwenyezi Mungu, ili waweze kushinda mapambano dhidi ya ibilisi anaye jiinua kwa njia nyingi ili kuwapoteza Wanadamu.

Kwa hisani ya Radio Maria, Tanzania.









All the contents on this site are copyrighted ©.