2013-03-30 11:12:26

Kesha la Pasaka kwa mwaka 2013 mjini Vatican


Kesha la Pasaka ni Usiku Mtakatifu ambao Mama Kanisa amekuwa akiuadhimisha kwa heshima kuu kadiri ya Mapokeo yake. Ni Usiku wenye utajiri mkuu wa maisha ya kiroho, mwaliko kwa waamini kuendelea kukesha huku wakisubiri ujio wa pili wa Yesu Kristo, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na kwamba, ufalme wake hauna mwisho. Usiku wa Pasaka ni kielelezo cha waamini kuvuka kutoka katika dhambi na mauti na kuanza hija ya maisha mapya katika Kristo Mfufuka.
Katika Kesha la Pasaka, Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka, aliyeshinda dhambi na mauti, ndiyo maana Mama Kanisa anathubutu kuimba sifa za Mshumaa wa Pasaka “Exultet” Yaani Mbiu ya Pasaka. Ni kesha lenye utajiri mkubwa wa Liturujia ya Neno la Mungu, inayowakumbusha waamini mchakato wa historia ya ukombozi wa mwanadamu, tangu kuumbwa kwa ulimwengu hadi Siku ya kwanza ya Juma, Yesu Kristo alipofufuka kutoka katika wafu, mwaliko wa kuwashirikisha waamini katika Fumbo la Pasaka kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na kwa wale waliokwisha kubatizwa basi, wanapata nafasi ya kurudia tena ahadi zao za ubatizo.
Baba Mtakatifu Francisko, katika Kesha la Pasaka, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, anatarajiwa kutoa Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu kwa Wakatekumeni kutoka Italia, Albania, Russia na Marekani. Wakristo hawa wapya wataungama imani na kushiriki katika Sala ya kuliombea Kanisa, sala ambayo inajulikana na wengi kuwa ni Sala ya Waamini.
Mwishoni, Waamini wanaadhimisha Liturujia ya Ekaristi Takatifu, ambamo Yesu Kristo, Mwanakondoo aliyeteswa, akafa na kufufuka anajitoa tena kuwa ni Ekaristi, chakula na kinywaji cha kiroho, changamoto kwa kila mwamini kuwa ni Ekaristi Takatifu kwa jirani yake, lakini zaidi kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali n anafasi yao katika maisha. Kwa namna ya pekee, waamini wanaoshiriki Ekaristi Takatifu, wanaalikwa kwa namna ya pekee, kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka kwa njia ya utakatifu wa maisha.
Kesha la Pasaka anasema Mshehereshaji mkuu wa Ibada za Kipapa, Monsinyo Guido Marini ni kilele cha Maadhimisho ya Siku tatu za Mafumbo ya Ukombozi, yaani Alhamisi kuu, Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu na kuhimiza huduma ya upendo na mshikamano wa dhati. Ijumaa kuu, Kanisa limefanya kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo. Siku kuu ya Pasaka ni chemchemi ya furaha na matumaini inayopata mwendelezo wake katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.








All the contents on this site are copyrighted ©.