Jumuiya ya Wayahudi wa Roma yatuma salam za Pasaka kwa Baba Mtakatifu Francisko
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Pasaka ya Wayahudi, alimwandikia ujumbe
wa matashi mema Rabbi Riccardo Di Segni, Mkuu wa Jumuiya ya Wayahudi mjini Roma, ambaye
pia amemtumia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa matashi mema kwa Maadhimisho ya Siku
kuu ya Pasaka kwa Mwaka 2013.
Rabbi Riccardo Di Segni anachukua fursa hii kumshukuru
Baba Mtakatifu Frncaisko kwa ujumbe na matashi mema aliyoiandikia Jumuiya ya Wayahudi
inayoishi mjini Roma na kumtakia kheri na fanaka wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu
ya Pasaka ambayo kwa Mwaka huu siku zimekaribiana sana, hali inayoonesha uhusiano
na tofauti zilizopo kati ya dini hizi mbili, ambazo katika historia, wakati mwingine
ukajionesha katika hali ya kinzani na Jumuiya ya Wayahudi kutovumiliwa.
Kurasa
hizi chungu zinaonekana kupitwa na wakati na sasa waamini wa dini hizi mbili wanafurahia
matunda ya imani yao, mwaliko wa kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani za dhati. Rabbi
Di Segni anasema, anasukumwa na moyo wa heshima, urafiki na udugu ili kumtakia mema,
kwa ajili ya mema yenyewe kwa kutambua tofauti zilizopo pamoja na kuendelea kuthamini
moyo wa udugu.