Ibada ya Ijumaa kuu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican
Mama Kanisa katika adhimisho la Ijumaa kuu anafanya kumbu kumbu ya mateso na kifo
cha Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Siku ya kufunga kama kielelezo cha nje kinachoonesha
ushiriki wa waamini katika mateso ya Yesu Kristo. Hakuna adhimisho la Fumbo la Ekaristi
Takatifu kwani Kristo ambaye ndiye chemchemi ya Sakramenti zote za Kanisa anateseka
na hatimaye, kufa Msalabani.
Ijumaa kuu jioni, Kanisa limeadhimisha Mateso
na Kifo cha Yesu, anayejionesha kuwa ndiye Mtumishi wa Mungu aliyetabiriwa na Manabii
katika Agano la Kale. Ni Mwana Kondoo wa Mungu anaye yamimina maisha yake kwa ajili
ya ukombozi wa wengi.
Msalaba ni alama kuu inayochukua kipaumbele cha pekee
katika Maadhimisho ya Ijumaa Kuu. Ni kielelezo cha Mti wa Ushindi wa Kristo dhidi
ya dhambi na mauti, ndiyo maana, waamini wamepata fursa ya kuweza kuabudu Msalaba
wa Kristo.
Mjini Vatican, Ibada ya Ijumaa kuu ambayo kimsingi imegawanyika
katika sehemu kuu tatu yaani: Liturujia ya Neno la Mungu inayohusisha mahubiri ambayo
kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican yametolewa na Padre Raniero Cantalamessa,
Mhubiri wa nyumba ya Kipapa pamoja na Sala za Waamini kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu
katika ujumla wake. Sehemu ya Pili ni Liturujia ya Ibada ya Kuabudu Msalaba na Sehemu
ya tatu ni Ibada ya Komunio Takatifu.