2013-03-29 08:50:36

Msimruhusu mtu yeyote yule kuwapokonya tena matumaini yenu!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Maadhimisho ya Karamu ya Mwisho kwenye Gereza la Watoto la "Casal del Marmo", amemshukuru Mama Paola Severino Waziri wa Mambo ya ndani wa Italia kwa niaba ya Serikali ya Italia. Kwa namna ya pekee, amewashukuru vijana waliohudhuria Ibada ya Misa Takatifu kwa kusema kwamba, amepata furaha kubwa sana moyoni mwake kwa kuweza kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja nao!

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko amewatia shime vijana hawa kusonga mbele kwa imani na matumaini mapya na kamwe wasitoe nafasi kwa mtu yoyote kuwapokonya matumaini walio nayo moyoni! Matumaini haya yawasaidie kusonga mbele kwa kujiamini zaidi.

Kijana mmoja mwenye ujasiri, amemuuliza Baba Mtakatifu Francisko, kwa nini ameamua kwenda kuwatembelea? Baba Mtakatifu amemjibu kijana huyu kwa kusema kwamba, alijisikia kutoka katika undani wa moyo wake kuja kuwatembelea na kuwafariji, kielelezo cha fadhila ya unyenyekevu na huduma inayopaswa kuoneshwa na Askofu.

Baba Mtakatifu anasema, wakati mwingine mambo ya maisha ya kiroho hayana maelezo ya kina, kwani huu ni msukumo kutoka katika undani wa mtu mwenyewe. Baba Mtakatifu Francisko amewaomba vijana hawa ambao wanatumikia adhabu zao gerezani humo, kumwombea katika maisha na utume wake.

Waziri wa Mambo ya ndani wa Italia, akihojiwa na Radio Vatican anabainaisha kwamba, maneno ya Baba Mtakatifu Francisko yamewagusa vijana hawa na kuacha chapa ya kudumu. Vijana wameonesha jicho la upendo wakati wote wa maadhimisho wa Karamu ya Mwisho ambayo Baba Mtakatifu ameamua kuiadhimisha kwenye Gereza la Watoto watukutu!

Amewaonjesha matumaini na kuwachangamotisha wahudumu wa magereza kuonesha upendo na moyo wa huduma kwa wafungwa waliomo gerezani. Hii ndiyo hali iliyojionesha pia katika macho ya Askari Magereza, Wafanyakazi, Wahudumu na watu wanaojitolea Gerezani hapo.

Huu ndio ujumbe unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko si tu kwa ajili ya Magereza ya Italia, bali Magereza yawe ni shule inayosaidia mchakato wa kuleta mabadiliko katika maisha ya mtu, ili baada ya kutumikia adhabu yake gerezani arudi na kujiunga tena na Jamii akiwa ni mtu mwema. Magereza yasiwe ni mahali pa mateso na mahangaiko ya watu! Utu na heshima ya wafungwa viheshimiwe na kuthaminiwa, licha ya makosa yao, bado wanaendelea kuwa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.