Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu ni Sakramenti Pacha!
Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi, Kenya, Alhamisi kuu, asubuhi,
ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta Matakatifu, kwenye Kanisa
kuu la Familia Takatifu, lililoko Jijini Nairobi. Kardinali Njue amewakumbusha Mapadre
kwamba, Upadre ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Kanisa lake. Mapadre
ni viongozi waliodhaminishwa utume wa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa, ambayo wanapaswa
kuwashirikisha waamini wao.
Kardinali Njue anasema kwamba, Sakramenti ya Daraja
Takatifu na Ekaristi Takatifu ni Sakramenti Pacha, kwani huwezi kuadhimisha Fumbo
la Ekaristi Takatifu bila ya kuwa na Padre na huwezi kupata Daraja Takatifu nje ya
Sakramenti ya Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu.
Mapadre katika ulimwengu mamboleo
wanaendelea kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wao, jambo
la msingi ni kuishi ile fadhila ya unyenyekevu pamoja na kujitoa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya Mungu na Jirani. Mapadre ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, wanapaswa
kukoleza na kung'ara kwa njia ya utakatifu wa maisha yao.
Mapadre wawasaidie
waamini kuifahamu imani, kuiadhimisha, kuimwilisha na kuisali, kama ushuhuda wa imani
tendaji katika hija ya maisha ya waamini hapa duniani. Mapadre wanayo dhamana kubwa
katika mchakato mzima wa Uinjilishaji Mpya, ili kuwasaidia waamini kuweza kuyatakatifuza
malimwengu, ili hatimaye, dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Katika
Maadhimisho ya Misa ya Krisma ya Wokovu, Mapadre wa Jimbo kuu la Nairobi, wamerudia
ahadi zao za utii kwa Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi.