2013-03-28 08:14:49

Njia ya Msalaba, ni kilio dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu, changamoto ya kukumbatia: amani, majadiliano, upendo na mshikamano wa dhati


Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Ijumaa kuu, Mama Kanisa anapofanya kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo Msalabani, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Njia ya Msalaba kwenye Magofu ya Coloseo yaliyoko mjini Vatican. RealAudioMP3

Tafakari ya Njia ya Msalaba yenye vituo kumi na vinne kadiri ya Mapokeo, imetolewa na Kardinali Bèchara Boutros Rai, Patriaki wa Kanisa la Kimaroniti, kwa ombi maalum kutoka kwa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.

Katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano, Patriaki Boutros Rai anabainisha kwamba, mawazo makubwa yaliyojitokeza katika tafakari ya Njia ya Msalaba kwa Ijumaa kuu ni mwaliko na changamoto ya kugundua kwa mara nyingine tena fadhila ya amani, mshikamano wa upendo kwa wote wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Hii ni tafakari iliyoandikwa na vijana kutoka Lebanoni wakiongozwa na Kardinali Boutros Rai.

Hawa ni vijana walioguswa na cheche za mtutu wa bunduki na kwamba, kifo daima kiko mbele ya macho yao. Wanaendelea kushuhudia mateso ya wananchi wa Syria na nchi jirani, ambako raia wanalazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita na hivyo kujikuta wakiwa wageni hata katika nchi yao wenyewe.

Ni watu wanaokabiliana na mateso, lakini bado wana matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi, baada ya kufanya tafakari ya kina kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo katika hija ya maisha yao kama Wakristo. Mateso kwa njia ya Kristo yanapata maana mpya, kwani haya ni kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Vijana wanasema, wote wanaoteseka wanaweza kuonja tena matumaini katika maisha yao kwa njia ya ufufuko wa Yesu Kristo kutoka katika wafu.

Patriaki Boutros Rai anabainisha kwamba, wazo la kuwapatia vijana wa Lebanon dhamana ya kuandika tafakari ya Njia ya Msalaba kwa Mwaka 2013 kutoka kwa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, ni kitendo cha kinabii kabisa. Papa Benedikto wa kumi na sita, aliwataka vijana kuonesha magumu na machungu wanayokabiliana nayo; matumaini na matarajio ya wananchi wanaoishi huko Mashariki ya Kati.

Ni tafakari zinazopata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu; mateso na mahangaiko ya wananchi walioko Mashariki ya Kati na Ulimwengu kwa Ujumla na mwishoni ni matumaini yao kwa Kristo. Hizi ni tafakari ambazo zimeandaliwa na Vijana katika makundi na Patriaki Boutros Rai, akahitimisha kazi hii kubwa kwa kuhariri yale ambayo vijana walikuwa wameyatafakari katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Njia ya Msalaba ni fursa makini kwa kila mwamini na wote wenye mapenzi mema kuweza kukutana na Kristo katika mateso yake kama binadamu. Kila kituo cha Njia ya Msalaba ni Mlango maalum wa kukutana na Yesu katika safari yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Uso wa Yesu Mteswa unaendelea kujionesha sehemu mbali mbali za dunia, changamoto na mwaliko kwa kila mwamini kuubeba vyema Msalaba wake kisha kumfuata Kristo, akijitahidi kugundua maana ya Mateso yanayokomboa. Lengo ni kutowakatisha tamaa wale wanaomfuasa Kristo, bali kila mwamini ajitahidi kukamilisha ndani mwake yale mateso yanayopungua kutoka kwa Kristo kwa ajili ya Kanisa lake.

Ni tafakari zinazogusa mahangaiko ya watu kutokana na vita, kinzani na migogoro ya kijamii; uvunjifu wa haki msingi za binadamu na ukosefu wa amani na usalama. Hadi sasa Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kutoa suluhu ya kudumu kutokana na mgogoro wa kivita unaoendelea huko Mashariki ya Kati. Yote haya ni matokeo ya misimamo mikali ya kiimani. Vijana wa Lebanon wameyaona na kuyafanyia tafakari ya kina.

Katika tafakari hii makini, Vijana wa Lebanon wameongozwa kwa namna ya pekee na Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Kanisa Mashariki ya Kati au kama unavyojulikana kwa Lugha ya Kilatini “ Ecclesia in Medio Oriente”. Hapa mkazo unawekwa zaidi kwenye umoja na mshikamano; majadiliano ya kidini na kiekumene na kwamba, kama waamini Imani inapaswa kupewa msukumo wa pekee katika maisha yao kama yalivyo pia matumaini.

Baada ya mateso na kifo, kuna ufufuko wa Kristo kutoka katika wafu! Hii inaonesha kwamba, kimsingi Ijumaa kuu haina maana sana, ikiwa kama Yesu Kristo hasingelifufuka kutoka katika wafu. Ufufuko wa Kristo ni ushindi dhidi ya dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu Francisko anashiriki kwa mara ya kwanza katika Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo kwa mara ya kwanza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hawa ni viongozi wa Kanisa ambao wameguswa kwa namna ya pekee na mateso pamoja na mahangaiko ya wananchi wanaoishi Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Lebanon kuanzia tarehe 14 hadi 16 Septemba 2012 alibahatika kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kikristo na Kiislam, akakazia umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia ya kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na upatanisho wa kweli.

Ni matumaini ya wananchi wa Mashariki ya Kati kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ataendeleza mchakato wa Kanisa kutafuta na kukoleza misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano na upatanisho. Papa Francisko tangu alipochaguliwa, alifafanua maana ya jina lake na hadi sasa ameonesha ule utashi wa kutaka kuwa karibu na kwa ajili ya watu.








All the contents on this site are copyrighted ©.