Jumapili ya huruma ya Mungu, Papa Francisko kuadhimisha Ibada kwenye Kanisa kuu la
Mtakatifu Yohane wa Laterano
Katika maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu, hapo tarehe 7 Aprili 2013, Siku
kuu iliyoanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kunako mwaka 2000, Baba Mtakatifu
Francisko ataadhimisha rasmi Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Yohane wa Laterano, ambalo ni Makao Makuu ya Jimbo kuu la Roma. Ibada hii itafanyika
majira ya saa 11:30 Jioni kwa Saa za Ulaya.
Baba Mtakatifu Francisko katika
Katekesi yake ya kwanza kwa waamini, mahujaji na wageni iliyofanyika kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwaomba waamini kwa namna ya pekee,
kumwombea, kwani anatambua kwamba, hata Yeye ni Mdhambi, lakini anatumainia huruma
ya Mungu.
Ibada ya huruma ya Mungu ilianzishwa na kuendelezwa na Mtakatifu
Faustina, ikawa ni changamoto kwa waamini wote kuwa kweli ni mashahidi wa huruma ya
Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Itakumbukwa kwamba, Mwenyeheri Yohane
Paulo wa pili, alifariki dunia jioni iliyotangulia Maadhimisho ya Jumapili ya Huruma
ya Mungu, kunako mwaka 2005.