2013-03-27 09:22:31

Vijana salini kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake!


Katika Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, Siku ya Vijana Kijimbo na mwanzo wa Juma kuu, linalowapatia Wakristo fursa ya kutafakari Mafumbo Makuu ya Ukombozi, Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi, Jumapili iliyopita tarehe 24 Machi 2013, aliwataka vijana kusali kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameonesha mapendo makuu kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu Francisko tangu akiwa nchini Argentina alikuwa na mapendo makuu kwa vijana na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ni kiongozi ambaye ana mguso wa pekee kwa vijana. Katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kardinali Njue aliwakumbusha vijana kwamba, tema iliyokuwa inaongoza Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 ni changamoto inayowataka vijana kujitosa kimaso maso kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.

Itakumbukwa kwamba, mji wa Rio de Janeiro, Brazil, utaanza kutimua vumbi kwa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani hapo tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013. Katika mahubiri yake Kardinali Njue amewataka vijana kujifunza kwa namna ya pekee, Maandiko Matakatifu, kuyatafakari na hatimaye kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yao kama wafuasi amini wa Kristo.

Haya ndiyo matumaini ya wazazi, walezi na viongozi wao wa Kanisa. Vijana imara na thabiti katika imani, matumaini na mapendo ni dalili njema ya kuwa na Mapadre na Watawa wanaoweza kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao.

Kardinali John Njue ambaye wakati wa uchaguzi mkuu nchini Kenya alikuwa anashiriki kwenye Conclave mjini Vatican na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akachaguliwa, amewapongeza vijana nchini Kenya kwa kulinda na kudumisha amani na utulivu wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi nchini Kenya.







All the contents on this site are copyrighted ©.