2013-03-27 07:45:23

Onesheni imani yenu kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya matendo ya huruma


Askofu mkuu Felix Alaba Job, wa Jimbo kuu la Ibadan, Nigeria, katika Maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2013, alitoa mwaliko wa pekee kwa waamini kuonesha imani yao kwa njia ya matendo ya huruma, kama kielelezo cha toba na wongofu wa ndani katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Hii ni changamoto iliyotolewa pia na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa kutangaza na hatimaye, kuzindua Mwaka wa Imani, akiwataka waamini kuonesha ile imani tendaji kwa njia ya matendo ya huruma.

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanakubali kumfuasa Yesu Kristo, Mlango wa Imani na kuimarishwa kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara na Ekaristi Takatifu, inayowachangamotisha kuwa ni Ekaristi kwa jirani zao; na askari shupaji wa Kristo kutokana na kuimarishwa na Roho Mtakatifu. Imani inapaswa kujionesha katika matendo ya huruma na maisha adili, jambo ambalo linalipambanua Kanisa na misaada inayotolewa na Mashirika ya Kimataifa.

Jitihada zote walizofanya waamini kwa kufunga na kusali; kutafakari na kuimwilisha tafakari hii katika matendo ya huruma, iwe ni fursa ya kuonesha ile imani tendaji katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, kama waamini wao ni viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa ambalo limejengwa katika msingi thabiti ambao ni Yesu Kristo Mkombozi wa dunia.

Taarifa ya habari iliyotolewa na Shirika la Habari za Kanisa nchini Nigeria, inasema kwamba, Askofu mkuu Felix Alaba Job, amewataka waamini kuhakikisha kuwa, wanajikita katika kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Watoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini kwani mwelekeo wa sasa unaonesha kupanuka kwa pengo kubwa kati ya maskini ambao ndiyo “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” na matajiri wanaoendelea “kula kuku kwa mrija”.

Hii inatokana na ukweli kwamba, ufisadi, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma umekuwa ni jambo la kawaida, hakuna tena mtu anayeshtuka kwani dhamiri za watu wengi zimekufa!

Askofu mkuu Felix Alaba Job wa Jimbo kuu la Ibadan, Nigeria, anasema, mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaovaliwa njuga na Mama Kanisa katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, unapania kwa namna ya pekee, kuwa ni chombo cha kurekebisha maisha ya Jamii; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea: utu na heshima ya binadamu; haki msingi, amani, utulivu na upatanisho wa kweli.

Kwa namna ya pekee, Wakristo wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutolea ushuhuda wa imani yao katika medani mbali mbali za maisha, kwa kuonesha maisha adili, utu na heshima ya binadamu aliyekombolewa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, iwe ni fursa kwa waamini kuendelea kutolea ushuhuda wa imani tendaji; inayopaswa kurutubishwa kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu na Matendo ya Huruma. Kila mwamini ajifunge kibwebwe kutafuta amani na kuikumbatia kama kielelezo cha maendeleo endelevu ya binadamu, nchini Nigeria na sehemu mbali mbali za dunia.








All the contents on this site are copyrighted ©.