2013-03-27 11:42:51

Mwaka mmoja tangu Benedikto XVI alipofanya hija ya kichungaji nchini Mexico na Cuba, 2012!


Wananchi wa Mexico na Cuba wanaikumbuka hija ya kichungaji iliyofanywa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuanzia tarehe 23 hadi 28 Machi 2012. Kwa wananchi wa Cuba, hii ilikuwa ni hija ya pili kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kutembelea nchini humo baada ya hija ya kihistoria iliyofanywa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili.

Tangu wakati huo, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika uhusiano kati ya Kanisa na Serikali. Kanisa limepewa dhamana kubwa zaidi ya kutekeleza utume wake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Cuba: kiroho na kimwili.

Majadiliano yenye tija ambayo kwa sasa yamekuwa ni mhimili mkuu wa uhuru wa kuabudu pamoja na kujenga utamaduni wa kuaminiana kati ya Serikali na Kanisa, mambo ambayo yamechukua kipindi kirefu kubadilika. Waamini wanamkumbuka kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa kushiriki pamoja nao katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 400 ya Uwepo wa Sanamu ya Bikira Maria wa upendo.

Ni ushuhuda wa kina unaotolewa na Bwana eduardo Delgrado Bermudez, Balozi wa Cuba mjini Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican. Anasema, kwamba, kwa hakika anamkumbuka Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kwa wema na unyenyekevu wake; maamuzi yake yameacha chapa ya kudumu kwa viongozi wengi duniani.

Wakati huo huo, Bwana Hèctor Federico Ling Altamirano, Balozi wa Mexico mjini Vatican, anasema, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita nchini Mexico ilikuwa ni ngumu, lakini imeacha ushuhuda wa kudumu mioyoni mwa wananchi wengi wa Mexico, ambao waliguswa na neema na matumaini ambayo Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita aliwapatia.

Uvunjifu wa sheria na wimbi kubwa la wahamiaji ni kati ya mambo ambayo yaligusiwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita wakati wa hija yake ya kichungaji na yanaendelea kufanyiwa kazi ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu nchini Mexico. Ni kiongozi ambaye amewaachia wananchi wa Mexico matumaini kwamba, hata kama wanakabiliana na matatizo na changamoto nyingi, lakini wanaweza kuzivuka zote hizi na hatimaye, kufungua ukurasa mpya wa maendeleo.







All the contents on this site are copyrighted ©.