"Msigeuze mgogoro wa kisiasa kuchukua sura ya kidini kwani ni hatari kubwa"
Askofu mkuu Diudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati
akihojiwa na Radio Ufaransa amebainisha kwamba, wananchi wanakabiliwa na hali ngumu
na wasi wasi wa maisha baada ya waasi wa kikundi cha Seleka kuuteka mji mkuu wa Bangui
na baadaye kutangaza kusitishwa kwa matumizi ya Katiba na kwamba, Bunge halina nguvu
tena.
Kumekuwepo na vitendo vya uporaji wa mali na mauaji ya watu wasiokuwa
na hatia, jambo ambalo Askofu mkuu Nzapalainga anasema, linamsikitisha sana. Anawaomba
vikosi vya waasi kulinda raia na mali zao na kuwajibika kikamilifu kwa vitendo vyote
wanavyoendelea kufanya nchini humo. Jumapili iliyopita, watu wengi waliporwa mali
zao. Askofu mkuu ameonya kwamba, mgogoro wa kisiasa usigeuzwe kuwa ni chanzo cha choko
choko za kidini nchini humo. Viongozi wa Vikosi vya waasi waliofanya mapinduzi wanapaswa
kukomesha vitendo vya uporaji wa mali ya wananchi na kuwafikisha wahusika kwenye mkondo
wa sheria.
Kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Nzapalainga amewataka wananchi kujiepusha
na chokochoko zinazoweza kupelekea kinzani na hatimaye vita vya kidini nchini humo.
Viongozi wa kidini waheshimiwe na kupatiwa ulinzi, kama ambavyo pia wananchi wanapaswa
kulindwa dhidi ya vitendo vinavyoweza kusababisha maafa makubwa.