Jipangeni sawa sawa kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi mkuu Zimbabwe!
Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe linawataka wananchi wa Zimbabwe kujiandaa kikamilifu
kushiriki katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu,
kwani hili litakuwa ni tukio muhimu sana katika maisha yao, kama ilivyokuwa kunako
mwaka 1980 walipojipatia uhuru wao kutoka kwa Mwingereza, wakapandisha bendera yao
wenyewe na kuanza kutembea kifua mbele kama watu huru!
Maaskofu wanasema, umefika
wakati wa kuachana na siasa za chuki na uhasama; uvunjifu wa misingi ya haki na amani;
vitisho na ubabe; ukosefu wa misingi ya ukweli na uwazi; uwajibikaji; rushwa na ufisadi
na badala yake, wananchi wa Zimbabwe sasa wanapaswa kufungua milango yao ili kuonesha
ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia.
Hivi ndivyo wanavyoandika Maaskofu Katoliki
Zimbabwe katika barua yao ya kichungaji, wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya mchakato
wa uchaguzi mkuu baada ya kupitisha kwa kura nyingi Muswada wa Katiba Mpya ya Zimbabwe
kwa kupiga kura ya maoni.
Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe linasema kwamba,
wananchi wengi wa Zimbabwe wanatumaini kwamba, uchaguzi mkuu wa Mwaka 2013, utakuwa
huru na wa haki na hivyo kuifanya Zimbabwe kuonekana tena katika ramani ya kimataifa,
baada ya kupitisha Katiba Mpya na kufanya mabadiliko makubwa katika medani mbali mbali
za maisha ya watu!
Tarehe 16 Machi 2013, Zimbabwe ilipitisha Katiba Mpya iliyoungwa
mkono na Rais Robert Mugabe pamoja na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai, ambao kwa miaka
mingi wamekuwa ni maadui kisiasa, waliolazimika kunako mwaka 2008 kuunda Serikali
ya Umoja wa Kitaifa.
Katiba Mpya ya Zimbabwe ina mabadiliko makubwa yanayolenga
kudhibiti madaraka ya Rais pamoja na kutetea haki msingi za binadamu. Matamko ya Rais,
yatapaswa kuungwa mkono na wabunge wengi katika vikao vya Bunge. Mabadiliko makubwa
yanatarajiwa kuanza kutekelezwa mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa uchaguzi
mkuu nchini Zimbabwe.
Maaskofu wanasema kwamba, uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2013
ni fursa nyingine muhimu kwa wananchi wa Zimbabwe kuonesha ukomavu na uvumilivu wa
kisiasa, wakitambua machafuko yaliyoibuka nchini humo na kupelekea maelfu ya watu
kuyakimbia makazi yao na Zimbabwe iliyokuwa imecharuka kwa maendeleo Barani Afrika,
ikajikuta ikisua sua kwa kuandamwa na kinzani pamoja na migogoro ya ndani. Matokeo
yake yalikuwa ni kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Miaka kumi iliyopita, wananchi
wengi wa Zimbabwe wamejikita wakielemewa zaidi na masuala ya kisiasa.
Umefika
wakati kwa wananchi wa Zimbabwe kuondokana na utawala mgando, rushwa na ufisadi; tatizo
la watu kuyakimbia makazi yao; sera na siasa za chuki na uhasama; ukabila na udini.
Kanisa Katoliki kwa upande wake, limeendelea kuwajengea wananchi uwezo wa kujenga
na kuimarisha utamaduni wa amani, haki na upatanisho, kama sehemu ya mchakato unaopania
kuponya madonda ya chuki, kinzani na migogoro ya kijamii iliyojitokeza miongoni mwa
wananchi wa Zimbabwe.
Lengo ni kuendelea kuimarisha haki, msamaha na upatanisho
wa kitaifa, ili hatimaye, wananchi waweze kujenga na kuimarisha utamaduni wa amani.
Umefika wakati wa kuvumiliana na kujenga mazingira yatakayoweza kuufanya mchakato
mzima wa uchaguzi kuwa huru na wa haki, kwa kujenga na kuimarisha amani na utulivu.
Vurugu na vitisho ni sumu kali dhidi ya demokrasia na utawala wa sheria.