2013-03-27 15:11:14

Baba Mtakatifu Francisko asema, Juma kuu si kipindi cha huzuni, bali ni mwaliko wa kuingia na kuzama katika fikra na utendaji wa Yesu!


Kwa mara ya kwanza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko ameendeleza utamaduni wa kutoa Katekesi kwa waamini, mahujaji na wageni wanaofika mjini Vatican, Jumatano. Katekesi ya Baba Mtakatifu imejikita katika Maadhimisho ya Juma kuu, ambalo Mama Kanisa amelianza kwa Maandamano ya Matawi, Jumapili ya Matawi.

Hiki ni kilele cha Liturujia ya Mwaka wa Kanisa, pale waamini wanapotafakari matendo makuu yanayoonesha upendo wa Mungu kwa waja wake. Yesu aliingia mjini Yerusalem ili kujitoa kikamilifu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Akawajalia wafuasi wake Mwili na Damu yake Azizi, kielelezo makini cha uwepo wake endelevu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Akajitoa kimaso maso kuteswa hadi kifo Msalabani, kama kielelezo cha utii na mapenzi ya Baba yake wa mbinguni. Huu ni ushuhuda wa hali ya juu unaoonesha ni kwa namna gani Yesu anawapenda watu wake, changamoto kwa waamini kufuata nyayo zake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Juma kuu ni mwaliko wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya jirani; wale wanaotamani kuonjeshwa ukarimu, upendo, faraja pamoja na kupatiwa msaada. Ni changamoto ya kujitoa katika ulimwengu ambao unawapatia baadhi ya watu uhakika na usalama wa maisha yao kama Yesu anavyosimulia katika Injili, yaani kuwaacha wale Kondoo 99 na kwenda kumtafuta Kondoo mmoja aliyepotea.

Juma Kuu si kipindi cha huzuni, bali ni mwaliko wa kuingia na kuzama katika fikira na utendaji wa Yesu. Hiki ni kipindi cha neema zinazotolewa na Yesu zinayowawezesha waamini kumwilisha Imani katika matendo kwa kufungua mioyo, maisha, Parokia, vyama vya kitume kuwatafuta wale waliopotea ili kuwaonesha mwanga na furaha ya imani kwa Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, ametambua uwepo wa wanafunzi wa vyuo vikuu vilivyoko mjini Roma, wanaoshiriki katika Kongamano la Wanafunzi Kimataifa lililoandaliwa na Shirika la Opus Dei. Anawaalika wanafunzi kuhakikisha kwamba, wanaishi kikamilifu Juma Takatifu, wakijitahidi kufuata nyayo za Kristo, kwa kuwashirikisha wengine mwali wa upendo wa Yesu, wale wote watakaokutana nao katika hija ya maisha yao; kiwe ni kipindi cha Ibada na ushuhuda wa imani katika matendo! Baba Mtakatifu amewatakia mahujaji wote wanaozungumza lugha ya Kiingereza Pasaka Njema.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa mahujaji na wageni wanaozungumza lugha ya Kiarabu, amewataka kuwa na ujasiri wa kumfuasa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka; wawashirikishe wengine furaha na mwanga wa imani.







All the contents on this site are copyrighted ©.