2013-03-26 11:53:18

Ushiriki wa wanawake katika Njia ya Msalaba!


Kanisa limekianza kipindi cha Juma kuu kwa Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi. Katika tafakari ya Njia ya Msalaba kwa mwaka 2013 iliyoandaliwa na Kardinali Bèchara Boutros Rai kutoka Lebanon, itakayotumika Ijumaa kuu kuzunguka Magofu ya Colosseo kuna vituo vitatu vya Njia ya Msalaba vinavyoonesha uwepo wa wanawake waliomsindikiza Yesu katika Njia ya Msalaba kuelekea Kalvari.

Kituo cha Nne cha Njia ya Msalaba, Yesu anakutana na Mama yake Bikira Maria, uchungu kama upanga unapenya moyo wake, ili kufumbua siri zilizokuwa zimefichika tangu zamani kadiri ya utabiri wa Manabii. Bikira Maria anakutana na Yesu ambaye uso wake ulikuwa umeharibika kutokana na mateso makali. Ni Mama ambaye alikubali kumpokea Neno wa Mungu, akamtunza tumboni mwake. Yesu anateseka kumwona Mama yake akiteseka kiasi kile, ili kufungua ukurasa mpya wa maisha ya mwanadamu.

Mateso kama haya ndiyo ambayo wazazi na watoto wanayokutana nayo hata leo hii katika ulimwengu mamboleo. Changamoto ni kuendelea kuziombea Familia zetu ili ziwe kweli ni chemchemi ya furaha, amani, upendo na matumaini na kamwe zisikate tamaa kwa taabu na magumu wanayokumbana nayo katika safari ya maisha yao. Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, iwe ni kielelezo makini cha kulinda na kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Kituo cha Saba, Veronika anaupangusa uso wa Yesu uliokuwa umetapakaa damu. Ni mwanamke jasiri anayeonesha ushuhuda wa imani na upendo wake kwa Yesu bila kuogopa macho na maneno ya watu! Ni changamoto ya kuonesha upendo kwa maskini na wote wanaoteseka, kwani wote hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kati ya wale wanaoteseka ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu, watu wasiokuwa na makazi bila kuwasahau wote wanaodhulumiwa.

Katika Njia ya Msalaba, Kituo cha Nane, Yesu alifarijiwa na Wanawake kutoka Yerusalemu. Hapa Jamii inakumbushwa kuwaheshimu na kuwathamini wanawake ambao utu na heshima yao imeinuliwa kwa namna ya pekee kwa Bikira Maria kupewa heshima ya kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa. Inasikitisha kuona kwamba, hata leo hii bado kuna wanawake wananyanyaswa na kudhulumiwa. Basi, kila mara wanawake wanapokutana na Yesu Msulubiwa, watambue kwamba, Yeye ni chemchemi ya matumaini, kimbilio na wokovu wao.

Kila mwamini ajiandae vyema kuadhimisha Juma kuu hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha pia Mwaka wa Imani. Tumwombee Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuwa na nguvu, imani, mapendo na matumaini anapoendelea kutekeleza utume wake kwa ajili ya Kanisa la Kristo na Ulimwengu kwa ujumla.







All the contents on this site are copyrighted ©.