2013-03-25 10:01:09

Ratiba elekezi ya Maadhimisho ya Juma kuu mjini Vatican yatakayomshikirikisha Baba Mtakatifu Francisko


Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa, Monsinyo Guido Marini anasema kwamba, Ratiba ya Maadhimisho ya Ibada za Juma kuu zitakazoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko zitakuwa kama ifuatavyo:

Tarehe 28 Machi 2013: Alhamisi kuu, Saa 3:30 Asubuhi, Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Misa ya Kubariki Mafuta Matakatifu, itakayofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Mafuta yatakayobarikiwa kwa ajili ya matumizi ya Ibada Jimbo kuu la Roma yataweza kupatikana kutoka kwenye Sakristia ya Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano.

Tarehe 29 Machi 2013: Ijumaa kuu, Saa 11: 00 Jioni; Siku ya Kumbu kumbu ya Mateso ya Yesu Kristo. Baba Mtakatifu Francisiko, atashiriki katika Ibada ya Liturujia ya Neno, Kuabudu Msalaba na Kupokea Ekaristi Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican

Tarehe 29 Machi 2013, Ijumaa kuu, Usiku saa 3:15: Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Coloseo. Itakumbukwa kwamba, tafakari ya Njia ya Msalaba kwa Mwaka 2013 inatolewa na Kardinali Bèchara Boutros Rai, Patriaki wa Kanisa la Wamaroniti kutoka Antiokia. Tafakari hii ni kilio dhidi ya kila aina ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ni mwaliko wa kutafakari kutoka katika dimbwi la kifo na kuanza hija ya maisha mapya.

Tarehe 30 Machi 2013: Kesha la Siku kuu ya Pasaka litaanza hapo saa 2:30 kwa Baba Mtakatifu Francisko kubariki moto na baadaye kuingia ndani ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa maandamano yatakaoongozwa na Mshumaa wa Pasaka, alama ya Kristo Mfufuka. Kanisa litaimba Mbiu ya Pasaka kutangaza sifa za mshumaa wa Pasaka. Itafuata Liturujia ya Neno la Mungu, Ibada ya Ubatizo pamoja na Ibada ya Ekaristi Takatifu.

Tarehe 31 Machi 2013 Siku kuu ya Pasaka: Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuanza Ibada ya Pasaka saa 4:15 Asubuhi. Baada ya Maadhimisho haya, atatoa Salam kwa Mji wa Roma na Dunia kwa ujumla, kama zinavyojulikana kwa Lugha ya Kilatini, Urbi et Orbi.

Kwa sasa hii ndiyo Ratiba Elekezi iliyotolewa na Mshehereshaji Mkuu wa Ibada za Kipapa, Monsinyo Guido Marini. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itakuwa nawe bega kwa bega ili kukujuza yale yatakayojiri katika Ibada hizi, unaweza pia kufuata matangazo haya kwa kutumia tovuti ya Radio Vatican kwa anuani ifuatayo:

www.radiovaticana.va








All the contents on this site are copyrighted ©.