2013-03-25 10:53:19

Maaskofu Kenya wanawatakia Wakenya wote: Umoja, Amani na Uhuru wa kweli!


Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, anaendelea kuwahimiza wananchi wa Kenya na Vyama vya Kisiasa kwa ujumla kuhakikisha kwamba, vinatoa nafasi kwa Mahakama kuu kuweza kutekeleza wajibu wake barabara baada ya mmoja wa wagombea uchaguzi mkuu uliopita nchini humo kukata rufaa kupinga matokeo ya Urais.

Kardinali Njue amemwomba pia Rais kukubaliana na masharti yaliyotolewa na Mahakama kuu ya Kenya, kama sehemu ya utekelezaji wa utawala wa sheria. Ni wajibu kwa vyama vya kisiasa wakati huu tete nchini Kenya, kujizuia kufanya maandamano yanayoweza kuleta vurugu na uvunjifu wa amani nchini Kenya. Hii inatokana na ukweli kwamba, wananchi wa Kenya wamechoshwa na vurugu na kinzani za kijamii, na wala si busara tena kuwashirikisha katika masuala ambayo wanapenda kuyapatia mgongo na kuanza ukurasa mpya wa maisha na maendeleo yao.

Shirika la Habari za Kanisa kutoka Afrika, CISA linasema kwamba, Maaskofu Katoliki Kenya wanawapongeza wananchi wa Kenya kwa kujitokeza kwa wingi kutekeleza haki yao msingi kama raia kwa kupiga kura kwa amani na utulivu, huku wakivumiliana kutokana na tofauti zao za kisiasa, dalili za ukomavu wa kidemokrasia. Maaskofu pia wanawapongeza Wakenya kwa kuonesha uvumilivu na busara wakati wa kuhesabu kura na hatimaye, matokeo yalipotangazwa, hii inaonesha kwamba, kwa hakika Wakenya ni wapenda amani.

Maaskofu wanavishukuru na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama, kwa kuonesha umakini katika mchakato wa uchaguzi mkuu; wanawapongeza wanasiasa walioshiriki katika uchaguzi mkuu na vyama vya kisiasa kwa ujumla wao. Wanawapongeza wale ambao tayari wamekubali kushinda na kushindwa katika uchaguzi uliopita na kwamba, vyombo vya upashanaji habari vimetekeleza wajibu wao barabara.

Askofu mkuu Zacchaeus Okoth wa Jimbo kuu la Kisumu, Kenya anasema, Maaskofu walikuwa na wasi wasi wa ujumbe na matamshi yalionesha chuki na uhasama wa kikabila yaliyokuwa yamezagaa kwenye mitandao yao ya kijamii. Inasikitika kuona kwamba, bado kuna chembe chembe za chuki za kikabila. Anawataka kuongozwa na dhamiri nyofu, daima wakitafuta na kudumisha tunu msingi zinazopewa kipaumbele na Nchi ya Kenya katika ujumla wake.

Maaskofu wanaendelea kukazia umuhimu wa kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa, wakati huu wanaposubiri uamuzi wa Mahakama kuu. Wakati huu wa Juma kuu na hatimaye, Kipindi cha Pasaka, iwe ni fursa ya kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa; upendo pamoja na uchaji wa Mungu. Maaskofu wanatakia wakenya umoja, amani na uhuru wa kweli mioyoni mwao!







All the contents on this site are copyrighted ©.