2013-03-25 09:27:09

Jumapili ya Matawi: Kielelezo cha Furaha; Changamoto ya Kumfuasa Kristo Msulubiwa na Vijana kujitosa kumtangaza Kristo hadi miisho ya dunia


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya Matawi, aliongoza umati mkubwa wa waamini waliokuwa wamefurika kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kushiriki katika Ibada ya Jumapili ya Matawi, kielelezo cha kuanza Juma kuu. Baba Mtakatifu anasema, Yesu alipoingia mjini Yerusalemu, wafuasi wake walitandaza nguo zao njiani, wakaimba nyimbo za kumsifu Mungu wakisema, Mbarikiwa anayekuja kwa jina la Bwana, Hosana, Juu mbinguni. Amani duniani kwa watu anaowaridhia.

Baba Mtakatifu anasema, umati mkubwa wa watu, furaha na baraka ni mambo yanayoashiria furaha ya ndani inayobubujika kutoka kwa Yesu Kristo, aliyeijaza mioyo ya watu matumaini. Hawa ni wale waliosahaulika, maskini na "akina yakhe pangu pakavu tafadhali tia mchuzi! Yesu aliyafahamu mateso na mahangaiko ya mwanadamu, akawaonesha uso wa huruma ya Mungu, aliyejinyenyekesha ili kuponya madhaifu ya binadamu: kiroho na kimwili.

Huyu ndiye Yesu anayewaangalia wote: matatizo, magonjwa na dhambi zao. Anaingia mjini Yerusalem akitaka kuwaonesha watu upendo wake mkuu, unaowakumbatia watu wote katika furaha. Hii ndiyo furaha ambayo waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameionesha wakati wa Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, kwa kumsindikiza Yesu, kwa kutambua kwamba, yuko kati yao, kama rafiki, ndugu na Mfalme anayeangazia mapito ya watu wake.

Yesu ni Mungu aliyejinyenyekesha na watu wanapaswa kumpokea kwa FURAHA, neno ambalo Baba Mtakatifu Francisiko amependa kulikazia katika mahubiri yake, kwa kuwataka waamini kuwa ni watu wenye furaha na kamwe wasikubali kukatishwa tamaa kwani hii ni furaha inayopata chimbuko lake kwa mwamini kukutana na Yesu Kristo ambaye anaendelea kufanya hija na wafuasi wake, hata katika nyakazi ngumu za maisha yao na pale wanapokutana na vizingiti.

Hapa ni mahali ambapo waamini wanapaswa kuwa makini zaidi kwani Mwovu Shetani anaweza kuwajia akiwa amejivika sura ya Malaika; kamwe waamini wasimsikilize wala kumfuata, bali waendelee kumsindikiza na kufuasa Yesu Kristo chemchemi ya furaha ya kweli.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, kamwe wasikubali kupokonywa tumaini linalobubujika kutoka kwa Yesu mwenyewe. Yesu ni Mfalme, aliyeonesha unyenyekevu wa hali ya juu kabisa, changamoto na mwaliko wa kumfuasa kwa imani na matumaini, huku wakiendelea kumtangaza kuwa ni Mkombozi wa Ulimwengu. Anaingia mjini Yerusalem kwa shangwe, ili aweze kutimiza unabii uliotolewa katika Maandiko Matakatifu, kwa kuteswa, kufa na hatimaye, kufufuka kutoka katika wafu. Kristo alikufa Msalabani, mwaliko kwa waamini kukumbuka kwamba, wanamfuasa Kristo Mfalme aliyetundikwa Msalabani.

Kwa kifo chakle Msalabani, Yesu amejitwika dhambi na mapungufu ya mwanadamu, akayaosha kwa njia ya Damu yake Azizi, huku akiwaonjesha waamini huruma na upendo wa Mungu. Lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, hata leo hii, bado kuna: vita, makosa ya jinai, kinzani za kiuchumi na kijamii inayoendelea kuwaathiri zaidi wanyonge. Watu wanaonesha uchu wa mali na madaraka; wanaendelea kuogelea katika rushwa na ufisadi; , migawanyiko pamoja na kuenzi utamaduni wa kifo na uharibifu wa mazingira, bila kusahau dhambi za kila mwamini mmoja mmoja.

Watu wanakosa upendo kwa Mungu, jirani na katika kazi ya Uumbaji. Msalabani, Yesu ameweza kukumbatia yote haya kwa njia ya upendo wake mkuu unaoshinda dhambi na mauti na hatimaye kuonesha ushindi kwa njia ya Ufufuko kutoka katika wafu! Huu ndio ushindi wa Kristo unaooneshwa na Fumbo la Msalaba. Ni chemchemi ya furaha kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Msalaba, watu wamekombolewa.

Baba Mtakatifu Francisiko aliwakumbusha waamini na mahujaji waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwamba, Jumapili ya Matawi kwa Mwaka 2013, ilikuwa pia ni Siku ya Vijana Kijimbo, kama sehemu ya Maandalizi ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani. Umati mkubwa wa vijana umeshiriki katika maandamano ya Jumapili ya Matawi, ili kushiriki Siku kuu hii ya Imani, kwa kuwashirikisha wengine ile furaha ya imani inayobubujika kutoka katika moyo wa ujana.

Vijana wamemsindikiza Mfalme anayependa hadi upeo kwa njia ya mateso na kifo cha Msalaba, changamoto kwa vijana kuhudumia na kupenda, bila kuuonea aibu Msalaba wa Kristo. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kujitosa kimasomaso kumshuhudia Kristo ambaye ni chemchemi ya furaha yao ya kweli; Yeye ambaye ameshinda ubaya kwa njia ya upendo. Vijana wanachangamotishwa kufanya hija ya Msalaba hadi miisho ya dunia; huku wakiendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Kwa njia ya Msalaba, Yesu amevunja kuta za utengano kati ya watu; na badala yake amewakirimia upatanisho na amani.

Baba Mtakatifu Francisiko amewahakikishia vijana kwamba, anaungana na watangulizi wake: Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili na Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika hija ya Njia ya Msalaba. Anatarajia kukutana na umati wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, hapo Julai katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013.

Huu utakuwa ni muda wa furaha na imani kwa vijana kuweza kuutangazia ulimwengu jinsi inavyopendeza kumfuasa na kutembea na Yesu Kristo, kwa kujiondoa katika ubinafsi wao, tayari kutangaza Injili ya Kristo. Baba Mtakatifu Francisiko amehitimisha mahubiri yake kwa kukumbusha mambo makuu matatu: Furaha; Msalaba na Vijana.

Anawaalika waamini kumwomba Bikira Maria aweze kuwafundisha kuwa ni watu wenye furaha kwa kukutana na Yesu Kristo, ili kushiriki upendo wake ambao aliushuhudia alipokuwa pale chini ya Msalaba. Waamini wajitahidi kuwa na moyo wa ujana katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa katika Juma Takatifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.