2013-03-25 07:32:17

Baraza la Makanisa Ulimwenguni lina mpongeza Askofu Mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Jumuiya ya Kiangalikani Duniani


Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ni kati ya viongozi wakuu wa kidini walioshiriki katika sherehe ya kumsimika Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury, ambaye ni Kiongozi mkuu wa Jumuiya ya Waanglikani Duniani.

Askofu mkuu Welby anakuwa ni Askofu wa 105 wa Jimbo kuu la Cantebury. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Anglikani ni kati ya wanachama waanzilishi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Dr. Tveit anampongeza Askofu mkuu Welby kwa kuonesha utashi wa kutaka kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaongoza Waamini wa Kanisa Anglikani, walioenea sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, ameonesha pia utashi wa kuendeleza majadiliano ya kiekumene, jambo ambalo linavaliwa njuga na Makanisa mengi katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.

Ni matumaini ya Dr. Tveit kwamba, Askofu mkuu Justin Welby, ataweza kushirikisha uwezo na mang’amuzi yake ya shughuli za kichungaji katika kukuza na kuendeleza mchakato unaopania kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano; upatanisho na majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani.

Katika hotuba yake mara baada ya kusimikwa rasmi kuliongoza Kanisa Anglikani, Askofu mkuu Welby amekazia umuhimu wa upatanisho, haki na amani, kwa kuangalia kwa umakini mkubwa mchango ambao umeendelea kutolewa na Makanisa mbali mbali duniani.

Huu ni msukumo unaopata chimbuko kutoka kwa Kristo mwenyewe anayewataka wafuasi wake, kujipa moyo na kamwe wasiogope kumshuhudia Kristo katika maisha yao; kwa kujikita katika maisha ya sala, ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa na Familia ya binadamu.








All the contents on this site are copyrighted ©.